Na Shomari Binda-Musoma
KLINIKI ya utatuzi na kusikiliza kero za migogoro ya ardhi kwa mkoa wa Mara itaendelea kusikilizwa kesho Musoma vijijini.
Huu ni muendelezo baada ya kuzinduliwa na mkuu wa mkoa wa Mara Said Mtanda novemba 21 kwenye uwanja wa shule ya msingi Mukendo manispaa ya Musoma.
Akizungumza na Mzaws Blog Kaimu Kamishina Msaidizi wa ardhi mkoa wa Mara Dickson Mwinuka amesema baada ya kumaliza kusikiliza manispaa ya Musoma wanakwenda vijijini kuwasikiliza wananchi.
Amesema kwa mujibu wa maelekezo ya viongozi wanaendelea kuwasikiliza wananchi na kutatua migogoro na kero wanazozipokea.
Mwinuka amesema maafisa ardhi wa mkoa na wilaya wamejiandaa kwenda kusikiliza katika Kijiji cha Busekera ili kumaliza migogoro itakayopokelewa.
“Tumemaliza kusikiliza manispaa ya Musoma na tunakamilisha kuitatua na kesho tutakuwa Kijiji cha Busekera kuendelea kuwasikiliza wananchi”
“Kwenye jamii utofauti unaweza kujitokeza hivyo ni jukumu letu kama wataalam kupokea na kusikiliza ili muafaka uweze kupatokana” amesema Mwinuka.
Mkuu wa wilaya ya Musoma Dk.Khalfan Haule anaarajiwa kuwepo eneo la kusikiliza migogoro itakayopokelewa na kuipatia ufumbuzi.
Wananchi wenye migogoro wametakiwa kujitokeza kutoa kero na migogoro waliyonayoi ili waweze kusikilizwa na kutatuliwa.