Na Mwandishi Wetu Katavi
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana amewasili mkoani Katavi kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi itakayokwenda sambambamba na kupokea taarifa na kukagua miradi ya maendeleo.
Katika ziara hiyo ya kikazi ameongazana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Shaka Hamdu Shaka na baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege Katavi Kinana amepokelewa na Wana CCM Mkoa wa Katavi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama Mkoa Beda Katani.
Baada ya kuwasili Kinana akiwa na Shaka wamepata nafasi ya kusailiamana na wanachama wa Chama hicho na kisha kupokea taarifa ya CCM na Serikali Mkoa wa Katavi.
Akipokea taarifa hiyo Kinana ameelezwa hali ya mwenendo wa Chama na Serikali na kwa sehemu kubwa ameambiwa hali ni shwari na kwamba viongozi wamekuwa na ushirikiano mkubwa hali inayofanywa utekelezaji wa Ilani kufanyika kwa kiwango cha kuridhisha.
Kwa mujibu wa ratiba Kinana ambaye ameanza ziara leo Julai 25 ,2022 akiwa mkoani hapa mbali ya kupokea taarifa ya Chama na Serikali atazindua mradi wa fremu 15 za biashara, pia atatembelea mradi wa fremu za vibanda 188.
Aidha Kinana atazindua kituo cha afya na kuzungumza na wananchi na wanachama, pia baadae atazungumza na WanaCCM na viongozi mbalimbali . Kinana atakuwa katika ziara ya mikoa ya Nyanda za Juu ukiwemo Mkoa wa Katavi na kisha kuelekea Mkoa Rukwa, Songwe na Mbeya.