Mwanza
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana amepokea malalamiko 13 ya wavuvi wa samaki katika Ziwa Victoria ikiwemo utitiri wa kodi pamoja na mateso wanayoyapata wavuvi wanapokuwa ziwani.
Kinana ameyasema hayo leo Septemba 5, 2022 wakati akizungumza na wavuvi wa samaki wa Kanda ya Ziwa kwenye ukumbi wa BoT, akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lengo lake kuu ni kuwasaidia Watanzania ili kipato chao kiendelee kuongezeka wanapofanya biashara. Tunapozungumzia sekta binafsi mara nyingi tunawafikiria wawekezaji wakubwa wa viwanda na wakati mwingine tunawafikiria hata watu kutoka nje pekee.
“Ieleweke ukiifikiria sekta binafsi ni hawa (wajasiriamali wadogo) na ndio wenye viwanda vidogo, wanajituma ili wawe na maisha bora. Serikali haiwezi kumwondolea mtu umasikini wake, lakini inaweza kutengeneza mazingira mazuri, sheria na kanuni nzuri ili iwe rahisi kwa mtu kufanya shughuli zake kwa ufanisi na kwa faida, hiyo ndio kazi ya Serikali,” amesema Kinana.
Amesema wakati anasikiliza risala ya wavuvi miongoni mwa malalamiko ni uwepo wa kodi 11 ambazo ili uweze kumudu lazima uwe na kipato kikubwa huku akieleza kushangzwa na uwepo wa kodi ya maegesho kwa vyombo vya uvuvi.
“Niwaambie nia ya Rais na nimemsikia Rais amezungumza juu ya malengo manne aliyonayo maana la kwanza ni kuleta maridhiano kwa Watanzania, kuleta maboresho ya serikali katika muundo, sheria, sera na kanuni ili maisha ya watu yawe bora zaidi.Sasa katika kuboresha mambo risala yenu hii itatizamwa namna gani tunaweza kubadili mambo yao yawe bora zaidi. Risala yenu itatazamwa namna gani tunaweza kubadilisha mambo ambayo yapo kama 13,” amesema.
Awali akisoma risala ya wavuvi, Katibu wa Kamati ya Ushauri wa Wavuvi Ziwa Victoria Mayalu Kasiri, alielezea changamoto na matatizo yanayosumbua sekta ya uvuvi na kusababisha kudorora.
Ametaja changamoto hizo ni kukithiri kwa uvuvi haramu, biashara holela ya mabondo ya Sangara, muundo wa Wizara ya Uvuvi ambapo ameeleza sio mzuri kwa kuwa ina mkurugenzi mmoja ambaye ndiye anayeratibu shughuli zote za wizara, Serikali kuweka mfumo rasmi wa wavuvi, changamoto ya uwepo wa tozo 11, ulinzi na usalama, bei kubwa ya dizeli, petrol na mafuta ya taa, sheria za uvuvi na kanuni zilizopo sasa ni kukandamiza wavuvi mazalia ya samaki katika ziwa victoria kuharibiwa, matumizi mabaya ya taa za sola na fidia kwa wavuvi walioathiriwa, operesheni sangara mwaka 2018 na mwisho ni kutokuwepo bodi ya uvivi ambapo wameomba iundwe ili kuratibu masuala ya uvuvi kwa ukaribu zaidi.
Mwisho