NA MWANDISHI WETU
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia zoezi la upandaji miti katika maeneo yao ili kufikia lengo lililowekwa na Serikali.
Pia, amewataka viongozi wa majiji na manispaa kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara Mijiji na Vijijini (TARURA) kuwa na miti ya kutosha kando ya barabara zinazopita katika maeneo yao ili kuhifadhi mazingira.
Dkt. Jafo ametoa kauli hiyo leo Januari 10, 2023 wakati akiongoza zoezi la upandaji miti kando ya barabara kuu eneo la CBE-Tambukareli jijini Dodoma ikiwa ni Wiki ya Maadhimisho ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Amesema baada ya nchi yetu kukumbwa na ukame katika baadhi ya maeneo ni vyema sasa wananchi wakatumia mvua hizi zinazoendelea kunyesha kupanda miti ya kutosha katika maeneo yetu na kwenye vyanzo vya maji.
“Viongozi twendeni tukasimamie wilaya zetu kwa kupanda miti milioni 1 na laki tano kwa kila halmashauri ili tufikie lengo la kupanda miti milioni 276, jambo hili tutalifanikisha kwa kutumia mvua hizi kupanda miti, hapa nataka niwapongeze Dodoma mmeonesha mfano na ndani ya miaka mitatu mtakuwa jiji la mfano kwa utunzaji mazingira,” amesema.
Akiendelea kuzungumza na wananchi pia Waziri Jafo amewataka wataalamu wa kilimo wabainishe aina za miti na washauri ipandwe katika maeneo gani ili kuepuka changamoto ya baadhi ya miti kufa.
Aidha, amewataka wakuu wa shule nchini kuhakikisha kila mwanafunzi anayeandikishwa shuleni kuhakikisha anapewa mti mmoja wa kupanda ili kuendana na Kampeni ya ‘Soma na Mti’ ambayo inalenga kupanda miti zaidi ya milioni 14.5.
Sanjari na hilo pia amesisitiza kila mwananchi anayeomba kibali cha ujenzi wa nyumba hakikishe anakuwa na mpango wa kupanda miti angalau mitatu na kuendelea ili tuwe na miti ya kutosha hivyo azma ya kupambana na athari z mabadiliko ya tabianchi itafanikiwa.
Zoezi la upandaji miti limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri, Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, viongozi wa Taasisi mbalimbali, Menejimenti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, wanafunzi,wadau wa mazingira na wananchi kwa ujumla.