Home Kitaifa KILA KAYA INATAKIWA KUWA NA CHOO BORA KUEPUKA KIPINDUPINDU

KILA KAYA INATAKIWA KUWA NA CHOO BORA KUEPUKA KIPINDUPINDU

Na. Majid Abdulkarim, WAF

Waziri wa Afya, Mhe Ummy Mwalimu amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo bora na kuzingatia unawaji mikono mara kwa mara ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu nchini.

Waziri Ummy ametoa agizo hilo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa kufungua mafunzo ya kujengeana uwezo wa kupambana na kipindupindu katika nchi za Tanzania, Malawi, Zambia, Msumbiji na Angola ambapo amebainisha kuwa tangu mwezi Januari mwaka huu Tanzania imerekodi visa 519 na vifo 11 vya ugonjwa wa kipindupindu.

“Hivyo Wakuu wa Mikoa na Wilaya hakikisheni mnaweka mbele Agenda ya kuzuia ugonjwa wa kipindupindu ambao hadi sasa umerekodiwa katika mikoa ya Katavi, Kigoma na Rukwa”, ameeleza Mhe.Ummy.

Akizungumza Waziri Ummy amesema halmashauri zinatakiwa kusimamia sheria za usafi na kuzuia utiririshwaji wa maji taka mitaani na hasa watiririshaji wa maji machafu wakati wa mvua wachukuliwe hatua kali za kisheria ikiwemo kuweka faini kubwa kuliko gharama za kuita gari la maji taka.

Waziri Ummy amesema kwa ujumla kipindupindu ni ugonjwa wa kimaskini na umasababishwa na maji machafu, chakula kichafu na kutozingatia kanuni za usafi.

“Kuanzia mwezi Januari, 2022 Hadi mwezi Agosti tumerekodi visa 519 vya ugonjwa wa kipindupindu katika mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma ambapo vifo vilivyotokana na ugonjwa huu ni 11”.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema kuwa Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wako tayari kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu kwa kuhakikisha wanasambaza maji safi na salama kwa kila kaya nchini.

“Jukumu letu kubwa sisi kama Wizara ya Maji ni kuhakikisha tunasababisha upatikanaji wa maji safi na salama ya kutosha katika maeneo yote ya makazi ya wananchi Pamoja na maeneo yote yanayotoa huduma za kijamii kama shule na hospitali”, amesema Mhandisi Mahundi.

Kaimu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani nchini Tanzania (WHO) Dkt. Zabulon Yoti amesema kipindupindu kinazuilika ikiwa mataifa haya matano yatawekeza katika usafi wa mazingira Pamoja na maji safi na salama kwa wananchi wao.

Akieleza Dkt. Yoti amesema Kipindupindu kinazuilika kabisa, hivyo kama tusipozingatia usafi wa mazingira Pamoja na maji safi na salama kitatusumbua.

“Vile vile amesema kuwa kama uwekezaji kwenye maji safi utawekewa nguvu na kipaumbele katika mamlaka basi tutaweza kutokomeza kabisa kipindupindu. Watu wengi kusini mwa Jangwa la Sahara hawana maji safi na hii ndiyo sababu hasa ya milipuko ya kipindupindu katika ukanda huu, mpango wetu ni kushirikiana na sekta za kimkakati kumaliza kipindupindu kufikia 2030 na hii itawezekana kwa kuwekeza kwenye maji safi na salama”- Dkt. Yoti

Mkurugenzi Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Meja Jenerali Michael Mmanga ametoa wito kwa wapanga miji kupanga miji katika namna ambayo itaweza kudhibiti maji machafu yasizagae mitaani na kusababisha mlipuko wa magonjwa ikiwemo huu wa kipindupindu, wahakikishe mitaro ina uwezo wa kumudu maji taka yasiingie kwenye makazi ya wananchi.

Aidha, Ugonjwa wa Kipindupindu ni ugonjwa ambao husababishwa na bakteria anayejulikana kama ‘Vibrio Cholerae’ ambaye hupatikana katika maji yasiyo safi na chakula kisicho salama pale mtu anapokula au kunywa chakula hicho. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2021 Afrika inawakilisha 20% ya visa vyote vilivyorekodiwa ulimwenguni, lakini cha kushangaa ni kwamba mbali na visa hivyo, 80% ya vifo vitokanavyo na kipindupindu kote ulimwenguni vimetokea Afrika huku sababu ikitajwa kuwa ni ukosefu wa maji safi na salama.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!