-WAJUMBE BODI YA BARABARA WAWAPONGEZA MENEJA TANROADS, TARURA
Na Shomari Binda-Musoma
WAKALA wa barabara nchini TANROADS Mkoa wa Mara wamekihakikishia kikao cha bodi ya barabara mkoa huo juu ya kupatikana kwa kibali cha kuendelea na ujenzi wa barabara ya Musoma-Makojo hadi Busekera kwa kilometa 42.
Uhakika wa kupatikana kwa kibali hicho umetolewa na meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara Vedastus Maribe wakati akiwasilisha makisio ya bajeti ya matengenezo na miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Amesema kibali kinapotolewa kwaajili ya kuendelea kwa ujenzi taratibu zinakuwa zimekamilika na inakuwa ni masuala madogo kwaajili ya ukamilishaji ili uweze kuendelea.
Maribe amesema kwa sasa Tanroads makao makuu moja ya mambo wanayoendelea nayo ni uandaaji wa makabrasha ili kuendelea kwa mradi.
“Nipende kukiambia kikao hiki mheshimiwa Mwenyekiti kibali juu ya uendelezaji wa ujenzi wa barabara ya Musoma-Makojo hadi Busekera kilometa 42 kwa kiwango cha lami”
“Barabara hii ni muhimu kwa wananchi wa Musoma vijijini na mkoa wa Mara kiujumla katika kusaidia masuala ya kiuchumi” ,amesema Maribe.
Meneja huyo amesema licha ya kuendelea na usimamizi wa miradi mbalimbali zipo changamoto ikiwemo wizi wa miundombinu zikiwemo taa za barabarani.
Akichangia kwenye kikao hicho cha bodi ya barabara mkoa wa Mara mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Profesa Sospeter Muhongo ameshauri kutenga miradi ya vipaumbele ili barabara ziweze kukamilika kwa wakati.
Muhongo amepongeza kazi zinazofanywa na Tanroads pamoja na Tarura kwa kazi wanazozifanya katika kuhudumia barabara.
Mkuu wa mkoa wa Mara Said Mtanda amesema ni vyema kwa sasa kukawa na ubunifu kwenye mizunguko ya barabara kuwa na nembo za vivutio vya mkoa wa Mara.
Amesema mkoa wa Mara una hifadhi ya ya Serengeti hivyo kwenye mizunguko hiyo unaweza kufanyika ubunifu kukawa na viti vya vivutio.