Home Kitaifa KATIBU MKUU GUGU ATAKA UFANISI WA HUDUMA ZA UHAMIAJI KUIMARISHA TASWIRA YA...

KATIBU MKUU GUGU ATAKA UFANISI WA HUDUMA ZA UHAMIAJI KUIMARISHA TASWIRA YA TANZANIA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu, amewataka maafisa wa uhamiaji kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuimarisha taswira ya nchi, hususan kwa wageni wanaoingia kupitia mipaka ya kimataifa.

Akizungumza jana wakati akifungua semina elekezi ya siku mbili kwa maafisa uhamiaji wa wilaya na wafawidhi wa vituo vikuu vya mipaka, iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) kilichopo mkoani Kilimanjaro, Gugu alisema maafisa hao ndio kioo cha taifa.

“Ninyi ndio taswira ya kwanza ambayo wageni wanakutana nayo, ikiwemo watalii, wawekezaji, na wafanyabiashara. Ni muhimu kuhakikisha mnatoa huduma bora itakayowafanya wageni wajisikie faraja kuwa nchini, jambo ambalo litachangia kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii na biashara,” alisema Gugu.

Aliongeza kuwa, kwa dunia ya sasa inayokwenda na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama), ni muhimu idara hiyo kuwekeza zaidi kwenye miundombinu ya kisasa ili kuboresha huduma. Alisema: “Serikali inatarajia maafisa wa uhamiaji wajenge hamasa ya kujiendeleza kitaaluma na kutumia teknolojia ili kuongeza ufanisi.”

Vilevile, Gugu aliwataka maafisa hao kusimamia kwa umakini ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kupitia huduma za uhamiaji, akisisitiza kuwa mianya ya rushwa na uchepushaji wa mapato lazima ikemewe. “Ukusanyaji mzuri wa maduhuli ni muhimu kwa maendeleo ya taifa letu,” alisema.

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (CGI), Dk. Anna Makakala, aliweka wazi kuwa semina hii ni sehemu ya utaratibu wa kila mwaka wa idara hiyo kufanya tathmini ya utendaji kazi na kujadili mipango ya maendeleo.

“Tumekuwa na vikao vya kila mwaka kwa maafisa wa mikoa, lakini mwaka huu ni kikao cha kwanza kwa maafisa wa wilaya na wafawidhi wa vituo vya mipaka. Kupitia vikao hivi, tumeimarisha umoja, uwajibikaji na ubunifu katika miradi ya maendeleo,” alisema Dk. Makalala.

Aliongeza kuwa kikao hicho pia kimewaleta pamoja makamishna wa uhamiaji, baadhi ya wakuu wa divisheni, na maafisa wastaafu kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujadili masuala muhimu kama vile uhusiano wa idara na jamii, maadili ya kiongozi, na nafasi ya idara hiyo katika diplomasia ya uchumi.

Dk. Makalala pia aliweka wazi kuwa washiriki watapata fursa ya kujadili mada mbalimbali ikiwemo rushwa, huduma bora kwa wateja, na afya ya akili kwa watumishi wa umma. “Tunatumia kikao hiki kama fursa ya kuboresha zaidi huduma zetu ili kukidhi malengo ya serikali ya awamu ya sita, ambayo inataka kuhakikisha usalama na maendeleo vinakwenda sambamba,” alisema.

Kuhusu utekelezaji wa majukumu ya uhamiaji, Dk. Makalala alisisitiza kuwa idara inaendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma ili kurahisisha udhibiti wa uingiaji, ukazi, na utoaji wa vibali na pasi. Pia, alieleza kuwa idara inaendelea kufanya oparesheni maalumu na misako kuhakikisha usalama wa taifa unaimarishwa.

Semina hiyo itafanyika kwa siku mbili ambapo washiriki watapata nafasi ya kufanya tathmini ya utendaji kazi na kufikia maazimio yatakayotekelezwa kwa mwaka ujao wa fedha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!