RC MTANDA ASHIRIKI IBADA MAALUM
Na Shomari Binda-Musoma
KANISA la New Life Gospel Community Church (NLGCC) maarufu kama “Bonde la Baraka’ lenye makao makuu mkoani Mara limeendesha ibada maalum ya kuliombea taifa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Ibada hiyo imefanyika kwenye Kanisa Kuu lililopo Musoma mjini na kuhudhuliwa na mkuu wa mkoa wa Mara Said Mtanda pamoja na viongozi mbalimbali na waumini wa Kanisa.
Akiendesha ibada hiyo,Askofu mkuu na kiongozi wa Kanisa hilo Askofu Daniel Ouma amesema taifa linahitaji maombi ili amani iliyopo iendelee kudumu katika kipindi chote.
Amesema bila kuwa na amani hakuna jambo lolote linaloweza kiendelea ikiwa ni pamoja na shughuli za kiuchumi wanazozifanya wananchi.
Askofu huyo amesema licha ya maombi kwa taifa juu ya amani lakini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Sluhu Hassan anapaswa kufanyiwa maombi ya pekee ili aendelee kuwahudumia watanzania.
Amesema kazi anayoifanya Rais Samia katika kuwaletea maendeleo watanzania ni kubwa hivyo ni muhimu kumuombea na kumuweka mikononi mwa Mungu.
“Tunaona namna Rais Dkt.Samia anavyofanya kazi kubwa katika kulisimamia taifa na watanzania na sisi kama Kanisa tumeona tumkabidhi mbele za Mungu.
“Hii ni ibada maalum ambayo tumeiandaa hapa bonde la baraka na tunaamini Mungu atapokea maombi yetu kwa namna tulivyomuomba“,amesema Dao.
Mkuu wa mkoa wa Mara Said Mtanda amesema Kanisa hilo limefanya jambo jema kwa kuandaa maombi hayo ambayo yana lengo jema kwa taifa na Rais Samia.
Amesema bila kumtanguliza Mungu kwenye kila jambo hauwezi kufanikiwa na kumshukuru Askofu Daniel Ouma”Nabii Dao) na Kanisa hilo kwa kuandaa ibada hiyo maalum juu ya kuliombea taifa na kiongozi wa nchi Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.