Na Edmund Salaho/Arusha.
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limezindua kampeni mahususi ya kupigia kura vivutio vyake viwili ambavyo ni Hifadhi ya Taifa Serengeti na Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro ambavyo vinashindanishwa kama vivutio bora zaidi barani Afrika, Kampeni inayoenda kwa jina la VOTE NOW”
Akizungumza na vyombo vya Habari wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo “VOTE NOW”
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara July Beda Lyimo alisema,
“Hifadhi ya Taifa Serengeti na Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro zimechaguliwa na Taasisi maarufu duniani ya World Travel Awards ikishindana na Hifadhi shindani kutoka Botswana, Namibia, Uganda, Afrika Kusini na Kenya, kwa upande wa Serengeti inashindana kama Hifadhi Bora Barani Afrika “Africa’s Leading National Park 2024” na kwa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro inashindana kama Kivutio Bora Afrika “Africa’s Leading Attraction 2024”.
Maeneo haya yamekuwa utambulisho wa Nchi ya Tanzania katika masuala ya Uhifadhi na Utalii kupitia Filamu ya “The Royal Tour” ambayo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alizitangaza Hifadhi za Taifa Serengeti na Kilimanjaro na kuiweka Nchi yetu katika Uso wa Dunia katika masuala ya Uhifadhi na Utalii ambapo kama Taifa tumeshuhudia matokeo chanya ya juhudi hizi za Mhe. Rais wetu.
“Tumekuja kwa watanzania wote, wadau wa utalii kuwaomba tupige kura kwa wingi ili hifadhi hizi ziwe kidedea na kuaminika kutokana na sifa za kipekee zilizojaliwa. Ushindi huo utaongeza idadi ya watalii, mapato kwa taifa na kuongeza ajira kwa watanzania” aliongeza Kamishna Lyimo.
Aidha, Kamishna Lyimo alisema kuwa, kuzipigia kura hifadhi hizi kuna faida kubwa kwa Taifa letu na vivutio vyake kwani vitaendelea kufahamika zaidi duniani na wageni wataendelea kuja kuvitazama kwa wingi zaidi na tutaogeza idadi ya mapoto kama ambavyo ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyotuelekeza kufikia watalii million tano na mapato ya dolla billioni sita ifikapo mwaka 2025.
Hifadhi ya Taifa Serengeti imeshinda tuzo hiyo ya Hifadhi Bora Barani Afrika kwa mara tano mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi mwaka 2023 ambapo kwa kura yako mwaka huu 2024 itaiwezesha Hifadhi hii kushinda kwa mara ya sita mfululizo huku Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro imeshinda tuzo ya kivutio Bora Barani Afrika mwaka 2013, 2015, 2016, 2017, na 2018 ambapo kwa kura yako tutaleta ushindi huu nyumbani kwa mara ya sita. Ili kupiga kura zako tembelea tovuti ya www.worldtravelawards/vote.