Home Kitaifa KAMISHNA WA TAWA AZINDUA MRADI WA JENGO LA OFISI LENYE THAMANI YA...

KAMISHNA WA TAWA AZINDUA MRADI WA JENGO LA OFISI LENYE THAMANI YA ZAIDI YA TZS MILIONI 250, AMPONGEZA RAIS SAMIA

Na. Beatus Maganja

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania – TAWA amezindua mradi wa jengo la ofisi lenye jumla ya vyumba 8 vikiwemo vyumba 6 vitakavyotumika kama ofisi, chumba cha mikutano, stoo pamoja na vyoo viwili, mradi unaotajwa kugharimu zaidi ya Tsh. Millioni 250.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jengo hilo iliyofanyika leo Januari 16, 2024 Makao Makuu ya Ofisi za Pori la Akiba Moyowosi zilizopo Kifura wilayani Kibondo Mkoa wa Kigoma, Kamishna Mabula amemshukuru Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiwezesha taasisi hiyo kukamilisha mradi huo na miradi mingine ambayo imekuwa na manufaa makubwa kwa TAWA.

“Tunamshukuru Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya kazi nzuri ya kutupatia fedha zilizotuwezesha kukamilisha mradi huu na miradi mingine tunayoitekeleza ikiwa ni pamoja na mishahara, yote hii ni matokeo ya Serikali yetu, ndiyo inayotuwezesha” amesema.

Aidha, Kamishna Mabula amewataka wahifadhi wa Pori la Akiba Moyowosi kuhakikisha wanalitunza vizuri jengo hilo ikiwa na pamoja na kuimarisha usimamizi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na TAWA ndani ya hifadhi hiyo.

Katika hatua nyingine, Kamishna huyo ameupongeza uongozi wa Pori hilo kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kulinda rasilimali walizopewa kusimamia kiasi cha kuwavutia wawekezaji.

“Nimefarijika sana wakati napokea taarifa yenu kujulishwa kwamba Pori la Akiba Moyowosi lina vitalu vya uwindaji wa kitalii 6 , na kati ya vitalu hivyo 6 vitano vina wawekezaji” amesema.

“Niseme tu kwamba hawa wawekezaji hawajaja bure wamekuja hapa kwasababu kuna rasilimali na hii rasilimali ipo kwasababu ya kazi yenu nzuri, mmefanya kazi nzuri ya kuhakikisha wanyama walioko kule porini na mazingira yao yako salama..kwahiyo niwapongeze sana kwa hilo” ameongeza.

Kwa upande wake Kamanda wa Pori la Akiba Moyowosi David Mnyapwani ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Menejimenti ya TAWA kwa jitihada za dhati za kuwezesha miradi inayotekelezwa katika Hifadhi hiyo kujengwa na kukamilika kwa wakati.

Ujenzi wa mradi huo ulianza kutekelezwa Mei 05, 2023 na kukamilika Septemba 09, 2023 na tayari umeanza kutumika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!