Home Kitaifa KAMISHNA MKUU WA TRA AHIMIZA ULIPAJI KODI WA HIARI

KAMISHNA MKUU WA TRA AHIMIZA ULIPAJI KODI WA HIARI

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amewataka watumishi wa Mamlaka hiyo kuendelea kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ya kusimamia ulipaji kodi wa Hiari.

Akifungua kikao cha nne cha Baraza la kwanza la Wafanyakazi wa TRA leo tarehe 04.03.2025 jijini Dodoma Kamishna Mkuu Mwenda amesema tangu alipoingia madarakani Rais wa awamu ya Sita alikuja na maelekezo mahususi kwa TRA ya kutaka kusiwepo na mabavu katika kukusanya Kodi.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema mbali na hayo Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kutoa maelekezo ya kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa na kuwachukulia hatua wale wanaojihusisha na ukwepaji wa Kodi kwa namna mbalimbali wachukuliwe hatua za kisheria.

Amesema kufuatia maelekezo hayo na miongozo inayotolewa wameweza kuongeza makusanyo ya kodi na kuvuka malengo waliyowekewa na Serikali kwa miezi Saba mfululizo na kuwataka watumishi wa TRA kuendelea kuzingatia maelekezo hayo ili waendelee kuvunja rekodi ya makusanyo.

Kamisha Mkuu Mwenda ametaja miongoni mwa mambo yaliyowawezesha kuvuka malengo kwa miezi Saba mfululizo kuwa ni pamoja na ulipaji wa Kodi wa Hiari unaohusisha utolewaji wa Elimu kwa Mlipakodi na ziara za Viongozi kuwafuata Walipakodi na kuwasikiliza hali ambayo imewezesha kutatuliwa papo kwa hapo kwa changamoto za Walipakodi.

Pamoja na wenzangu ndani ya TRA wakiwemo mameneja wa mikoa tumekuwa na utaratibu wa kuwafuata Walipakodi na kuzungumza nao katika maeneo yao hii imetusaidia sana kutengeneza uhusiano wa karibu na Walipakodi, na Mimi binafsi nimepita mikoa yote na nimekutana na Walipakodi” amesema Kamishna Mkuu Mwenda.

Amesema uhuru uliotolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa TRA kufanya kazi zao bila kuingiliwa unapaswa kutumiwa ipasavyo kwa watumishi kujituma na kuhakikisha mianya yote ya ukwepaji kodi inazibwa hali ambayo itaendelea kuimarisha makusanyo ya kodi na kuleta usawa katika kukusanya Kodi.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema mapambano dhidi ya wakwepa Kodi yanapaswa kuongezeka ili kutowaumiza walipakodi waaminifu ambao wamekuwa wakifanya kazi zao katika sehemu moja na wasiolipa kodi jambo ambalo linapunguza ushindani wa kibiashara hali inayoweza kuua Biashara za Walipakodi waaminifu.

Awali akizungumza katika kikao hicho, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mcha Hassan Mcha amesema Baraza la Wafanyakazi ni chachu ya kuboresha utendaji kazi na kuwa kwa kipindi cha muda mfupi ambao Baraza hilo limekuwepo, manufaa yake yameonekana.

Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Wafanyakazi la Mamlaka ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yahaya Kailembo amesema tangu kuanzishwa kwa Baraza hilo miaka mitatu iliyopita wameweza kushughulikia changamoto mbalimbali za wafanyakazi na kuisaidia Mamlaka kutimiza wajibu wake.

Kaulimbiu katika Mkutano huo wa Baraza la wafanyakazi wa TRA ni “Baraza la Wafanyakazi ni chachu ya utendaji kazi wenye tija, maadili na utumishi endelevu

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!