Na Mwandishi Wetu, Ngorongoro.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Richard Kiiza ameendelea na ziara ya kukagua zoezi la uelimishaji, uandikishaji na uthaminishaji wa mali za wananchi wa Ngorongoro wanaoendelea kuhamasika na kujiandikisha kuhama kwa hiari ndani ya hifadhi.
Wananchi hao wameendelea kuhamasika kuhama kwa hiari kwenda nje ya hifadhi hasa Kijiji cha Msomera na maeneo mengine waliyochagua wenyewe kwa lengo la kupisha shughuli za uhifadhi na kwenda maeneo ambayo serikali imewajengea miundombinu ya kisasa kama shule, maji, barabara, zahanati, umeme, mawasiliano, huduma za posta, majosho, malisho na mashamba ya kilimo.
Mtendaji wa Kijiji cha Kapenjiro kata ya Naiyobi Mejisho Mollel amemueleza kamishna Kiiza kuwa hadi sasa katika Kijiji chake zaidi ya kaya 235 zimeshajiandikisha kuhama katika Kijiji hicho na muamko wa wananchi wanaotaka kuhama umeendelea kuwa mkubwa kadri siku zinavyoenda.
Diwani wa Kata ya Naiyobi tarafa ya Ngorongoro Mhe. Ngeresa Reteti anaeleza kuwa wananchi wa kata hiyo wameendelea kuhamasika kujiandikisha kuhama hasa baada ya Serikali kuweka utaratibu mzuri wa wananchi kujiandikisha kwenye Ofisi za Kijiji na kuhakikisha kuwa wanaoandikishwa na kufanyiwa tathmini ya mali zao wanahamishwa ndani ya muda mfupi bila kukaa muda mrefu.
Kwa upande wake kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Richard Kiiza anabainisha kuwa kwa sasa Serikali imeboresha utaratibu wa kuelimisha na kuwaandikisha wananchi kwa kuwafuata sehemu walipo na zoezi la kuwaandikisha linapokamiliaka malipo huandaliwa haraka na ndani ya siku zisizozidi 10 taratibu zinakuwa zimekamilishwa na mwanachi kuhamishwa yeye na mifugo yake na kulipwa stahiki zake zote.
“Tunahakikisha kuwa mwananchi akiijiandikisha na kuthaminishiwa mali zake, ndani ya siku kumi (10) taratibu zote ikiwepo malipo zinakamilishwa ili mwanachi ahamishe bila kuchelewa, kwa sasa tumeongeza timu ya wataalam kutoka chou cha maendeleo ya Jamii ili kuwafikia kwa haraka wananchi wanaotaka kujiandikisha bila kuwachelewesha” amefafanua Kamishna Kiiza.