Home Kitaifa KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YARIDHISHWA NA UJENZI WA CHANZO KIPYA CHA...

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YARIDHISHWA NA UJENZI WA CHANZO KIPYA CHA MAJI BUTIMBA

Kamati ya kudumu ya bunge kilimo,mifugo na maji ikiongozwa na makamu mwenyekiti mhe Almas Maige wametembelea chanzo kipya cha uzalishaji maji Butimba ambacho kinatarajia kutoa lita milioni 148 kwa awamu ya kwanza, na baada ya kukamilika kwa awamu ya pili kitakuwa na uwezo wa kutoa lita milioni 160.

Kamati hiyo imeridhishwa na ujenzi wa chanzo hicho kipya cha uzalishaji maji kinachojengwa katika kata ya Butimba Wilayani Nyamagana Mkoani Mwanza ambacho kikikamilika kitatoa lita milioni 160 na kisha kuhudumia wakazi laki tano.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima amesema, mkoa huo una miradi ya maji yenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni mia tatu ikiwemo iliyokamilika pamoja na inayoendelea na utekelezaji lengo ikiwa ni kumaliza changamoto ya maji huku mkoa huo ukiwa na upungufu wa maji lita milioni 70

Mbunge wa Jimbo la Arusha Mrisho Gambo ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo amemtaka mkandarasi kutekeleza mradi huo kwa weledi na kuzingatia makubaliano ya mkataba wake ukizingatia ulitakiwa kuwa umekamilika mwezi desemba mwaka jana.

Kwa upande wake mbunge wa viti maalumu kutoka Dodoma Kunti Majala ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo amesema mradi huo umefikia asilimia 62 huku akisema tayari mkandarasi ameishalipwa fedha za utekelezaji wa mradi huo kwa asilimia 59 na kumtaka kuongeza kasi zaidi katika utekelezaji wake

Nae Naibu Waziri wa Maji Marryprisca Mahundi amesema kama wizara wamepokea maelekezo yote waliyopewa na kamati hiyo ili kuhakikisha yanafanyiwa kazi na mradi huo uweze kukamilika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!