Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizopo chini ya Ofisi hiyo.
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Florent Laurent Kyombe akikaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo hii leo Machi 19, 2024 katika Ofisi za Bunge Jijini Dodoma mara baada ya wajumbe kujadili na kuridhia bajeti katika kikao kilichohusisha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo, wataalamu kutoka Idara na Vitengo vya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Alieleza kuwa bajeti ya Ofisi hiyo iwe yenye matokeo changa na kusaidia kuleta maendeleo kwa wananchi huku akiipongeza Ofisi kwa kazi kubwa ya uratibu wa Shughuli za Serikali.
“Kipekee Kamati imepitisha makadirio ya bajeti hii muhimu mara baada ya kusikia wasilisho na kujadili kwa kina, tunashukuru kwa wasilisho endeleeni na jukumu la uratibu wa shughuli za Serikali kwa manufaa ya jamii katika kujiletea maendeleo,” alisema Makamu Mwenyekiti huyo.
Awali akiwasilisha taarifa kuhusu Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 mbele ya kamati hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama ameishukuru kamati kwa kujadili na kupitisha makadiri ya bajeti hiyo huku akisema Ofisi yake itaendelea kufanya kazi kwa weledi zaidi kwa kuzingatia jukumu la msingi la Uratibu wa Shughuli zote za Serikali.
Pia Waziri Mhagama alisema mpango wa shughuli zitakazotekelezwa kwa kutumia bajeti hiyo ya mwaka wa fedha ujao 2024/25 ambapo wanakamati kwa kauli moja walipitisha makadirio ya bajeti hiyo.
“Ni imani yangu kuwa bajeti hii itakapopita tunakwenda kutekeleza malengo yetu huku tukihakikisha shughuli mbalimbali ikiwemo za uratibu wa masuala ya maafa, uratibu wa shughuli za bunge, masuala ya tathmin na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali pamoja jukumu la uendelezaji wa Mji wa Serikali Mtumba Dodoma unaendelea vizuri ikiwa ni moja ya majukumu katika kuratibu,” Alisema Mhe. Mhagama
Akizungumza kuhusu masuala ya Ofisi ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali alihakikishia Kamati kuwa wataendelea kuboresha mitambo na kuisimamia vyema ili kuhakikisha kila nyaraka za Serikali ziendelee kuchapwa kwa Mpigachapa Mkuu wa Serikali.
=MWISHO=