Home Kitaifa KAMATI YA BUNGE YASISITIZA MRADI WA MAJI NZUGUNI KUKAMILIKA KWA WAKATI

KAMATI YA BUNGE YASISITIZA MRADI WA MAJI NZUGUNI KUKAMILIKA KWA WAKATI

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa maji uliopo Kata ya Nzuguni, jijini Dodoma jana Septemba 22, 2022.
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph wakati akitoa taarifa ya mradi wa maji uliopo Kata ya Nzuguni, jijini Dodoma jana Septemba 22, 2022 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo iliyofanywa na kamati hiyo.
Wananchi wa Kata ya Nzuguni wakichota maji kwenye moja ya kisima cha maji kati ya visima vitano ambavyo vimechimbwa katika Kata hiyo kwa thamani ya Shilingi bilioni 4.56 ili kutatua changamoto ya maji kwenye eneo hilo. Mradi huo unatarajiwa kukamilika baada ya miezi sita.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeisisitiza Wizara ya Maji na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kumaliza kwa wakati au kabla ya wakati mradi wa maji unaotekelezwa katika Kata ya Nzuguni iliyoyopo jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma ametoa rai hiyo jana jijini Dodoma wakati kamati hiyo ilipofanya ziara ya kutembelea mradi huo wa maji unaotarajiwa kuhudumia wananchi takriban 33,000 wa Mitaa ya Nzuguni, Ilazo na Kisasa.

Mhe. Dkt. Ishengoma amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuijali sekta ya maji na kujitahidi kutatua changamoto za maji hasa kwa wakati huu ambao miji mingi inakuwa na kusababisha ongezeko la watu.

Leo tumetembelea eneo hili la Nzuguni ambalo wananchi wake walikuwa na changamoto kubwa ya maji, hatimaye tatizo hili linaenda kutatuliwa kupitia visima hivi vitano vilivyochimbwa vinavyotoa maji safi na salama yasiyo na chumvi. Nawaomba mmalize mradi huu ndani ya miezi sita mliyoahidi au kabla ya miezi hiyo ili wananchi wasiendelee kuteseka na kero hii”, alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Kwa upande wake Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amesema kuwa wizara hiyo iliwaelekeza Wataalam wake kuyatafuta maji popote yalipo ili kuhakikisha Kata ya Nzuguni inaondokana na ukosefu wa huduma za maji safi, salama na yenye kutosheleza.

Wataalam wetu wamefanya kazi nzuri ambayo inatupa matumaini kuwa tatizo la maji katika Kata hii linakaribia kutatuliwa kwani mahitaji ya maeneo haya ni jumla ya lita milioni 4 na mradi huu unatarajiwa kuzalisha lita milioni 6, hivyo tutakuwa na maji yanayotosheleza.

Ameongeza kuwa Wizara inahakikisha fedha za mradi huu zitaendelea kutoka kwa wakati na imewaelekeza DUWASA kuhakikisha wanaaanzisha mradi mkubwa wa kujenga tanki litakalohifadhi lita milioni mbili na kutandaza mtandao wa mabomba wa zaidi ya Kilomita sita.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph amesema mradi huo wa maji Nzuguni umegharimu Shilingi bilioni 4. 56 na una faida nyingi ikiwemo ya kuongeza uzalishaji wa maji jijini Dodoma kutoka lita milioni 67.8 hadi lita milioni 73.8 kwa siku sawa na ongezeko la asilimia 9.

Pia mradi huu utaondoa mgao wa maji katika maeneo hayo na itasaidia maji yaliyokuwa yanahudumia Nzuguni kuelekezwa maeneo mengine ya karibu na chanzo cha Mzakwe yakiwemo ya Njedengwa, Mapinduzi, Mlimwa ‘C’, Iyumbu, Mwangaza, Swaswa na Ipagala wakati tukiendelea kusubiri kukamilika kwa miradi ya maji kutoka bwawa la Farkwa, Mtera na ziwa Victoria”, alimalizia Mhandisi Aron.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!