Home Kitaifa KAMATI YA BUNGE: HAKUNA MUDA WA KUONGEZWA UJENZI WA DARAJA LA JPM...

KAMATI YA BUNGE: HAKUNA MUDA WA KUONGEZWA UJENZI WA DARAJA LA JPM (KIGONGO – BUSISI)

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Balozi Mhandisi Aisha Amour amemtaka mkandarasi anayejenga mradi wa Daraja la JPM ( Kigongo- Busisi) Mkoani Mwanza kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili wananchi ambao wameusubiri kwa muda mrefu waanze kuutumia.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa Ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma ikiongozwa na Mwenyekiti wake Jerry Silaa ilipotembelea mradi huo mkoani Mwanza na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi na kisha kuridhishwa na utekelezwaji wake.

Mradi huu haujawahi kusimama kwa kukosa fedha hivyo namwagiza mkandarasi ahakikishe ifikapo February 24, mwaka 2024 awe ameukamilisha kwa ubora kama ilivyo kwenye mkataba,tunashukuru sana kamati hii kufika hapa kwenye mradi kuutembelea na kuukagua maana mnawawakilisha wananchi hivyo wakisikia kutoka kwenu watajua kwamba kazi inaendelea, amesema Mhandisi Amour.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini mhandisi Rogatus Mativila ameaihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuwa ujenzi wa Daraja la JPM ( Kigongo – Busisi ) utakamilika kwa wakati ifikapo February 24, mwaka 2024 kama ilivyokuwa katika mkataba wake.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jerry Silaa amesema kamati yake imeridhishwa na utekelezwaji wa mradi huo ambao unagharimu Sh Bilioni 716.33 na kufikia asilimia 70 ya utekelezwaji wake ambao unagharamiwa na serikali kwa asilimia 100.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo ameisisitiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuendelea kusimamia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ili daraja hilo likamilike kwa wakati wananchi wawe na uhakika wa kuvuka Ziwa Viktoria kwa urahisi wakitumia dakika nne badala ya Saa mbili wanazotumia sasa.

“Nasisitiza tena daraja hili linajengwa kwa fedha za serikali tunaomba likamilike Feb 2024 kama ilivyo kwenye mkataba wake, hakika tunaipongeza sana serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan hakuna mradi uliosimama na maendeleo yote yanayofanyika yanafanyika katika kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM),”amesema Silaa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!