Home Kitaifa KAMATI YA AMANI YAMPONGEZA RAIS SAMIA

KAMATI YA AMANI YAMPONGEZA RAIS SAMIA

KAMATI ya Amani na Jumuiya ya Maridhiano Tanzania imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka miwili madarakani na kusema katika kipindi hicho kwa kiasi kikubwa ameifungua Tanzania katika mambo mbalimbali ikiemo uhusiano wa kimataifa, Demokrasia na ukuaji wa Uchumi kupitia ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati.

Akizungumza Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Sheikh Alhad Mussa Salumu amesema kwa aliyoyafnya katika kipindi hicho cha miaka miwili kinapaswa kupongezwa na watanzania wote kwani kimeiletea Tanzania matunda kiasi cha kumfanya kila mtu kijivunia uwepo wake huku akiamini kuwa katika kipindi cha uongozi wake kinachoendelea atazidi kufanya mambo makubwa Zaidi.

Kuhusu kuifungua nchi Kidemokrasia, Sheikh Alhad amesema tofauti na huko nyuma kwa sasa wanasiasa wote wana furaha  baada ya uwepo wa maridhiano ya kisiasa na kuwafanya kuwa na amani na  kuondoa uoga uliokuwepo wa kufanya siasa zao katika maeneo mbalimbali ya nchi kama watanzania.

“Kwa hilo hana mpinzani, sote tumeshuhudia  Mheshimiwa Rais amefungua eneo la siasa na kuifanya Demokrasia kwamba sasa imekuwa pana huu ni ukomavu wa kisiasa, hata alipoudhuria mkutano wa Bawacha alipangua hoja baada ya hoja ya Mbowe na kuwasisitiza kila mmoja kushiriki kuijenga nchi, hizi ndizo habari ambazo kila mtanzania anapenda kuisikia” amesema Sheikh Alhad.

Amesema katika suala zima la haki, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kiasi kikubwa amewezesha kuwaonyesha watanzania ukomavu wa kisiasa ikiwemo kurahisisha utatuzi wa kesi mbalimbali zikiwemo za wanasiasa na watu wengine waliokuwepo katika vifungo magerezani jambo ambalo limewafanya watanzania wengi kufurahia na kurudi kuijenga nchi yao.

Kuhusu ushirikiano wa Tanzania kimataifa amesema ndani ya miaka miwili imeshuhudiwa Tanzania ikitembelewa na viongozi wa kimataifa na idadi kubwa ya watalii ambao wengi wao wamevutiwa na filamu ya ‘Royal Tour’ ambayo yeye mwenyewe Rais Samia Suluhu Hassan ameshiriki kuicheza jambo ambalo kiongozi huyo amesema kuwa halijawahi kufanywa na viongozi wengine waliopita katika Taifa hili.

Mbali na hayo kiongozi huyo wa juu wa Kamati ya Amani na Jumuiya ya Maridhiano amesema katika kipindi cha miaka miwili cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Tanzania imeshuhudiwa ikiwa katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo Reli ya kisasa (SGR), Barabara, Bwawa la kufua Umeme la Nyerere, Madaraja, Shule, Hospitali na miundombinu mingine.

Aidha amewataka watanzania wote wakiwemo wanasiasa kuendelea kumpa ushirikiano wa kutosha Rais Samia ili kumuwezesha kutimiza malengo yake  ya kulijenga Taifa na kuwaletea maendeleo watanzania katika kipindi chote atakaloliongoza Taifa hili na kwamba kwa kufanya hivyo kutaiwezesha Tanzania kupiga hatua zaidi za kimaendeleo.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Amani na Jumuiya ya Maridhiano Tanzania Mchungaji Geogre Fupe amesema uongozi wa miaka miwili wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani umegusa nyanja zote zinazopaswa kuwa kama msingi kwa Taifa lolote ikiwemo uwepo wa demokrasia imara, maendeleo ya ukuaji wa uchumi pamoja na uhusiano wa kimataifa.

Amesema katika kipindi hicho cha miaka miwili, Rais Samia Suluhu Hassan ameweza kuyasimamia hayo yote na kuifanya Tanzania kama nchi kufungua mipaka yake tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma na hivyo kuwavutia watu kutoka mataifa mengine kwa kuiona Tanzania sasa kama kimbilio lao.

Naye Katibu wa Jumuiya hiyo Askofu Islael Gabriel Masa, pamoja na mambo mengine  pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua yake ya kusimamia haki ya Mungu kwa kupinga ndoa za jinsia moja na kudai kuwa kama viongozi wa dini wanamuunga mkono katika hilo na kuahidi kuendelea kumpa ushirikiano wa kutosha wakati wote anapoliongoza Taifa hili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!