Theophilida Felician Kagera.
Mkoa Kagera ukiwa ni miongoni mwa mikoa yenye kukabiliwa na changamoto ya maambukizi ya ugonjwa tishio wa malaria mratibu wa malaria Mkoa Dkt Carlos Christian Jackison amesema jitihada mbalimbali zinaendelea ili kuweza kuudhibiti ugonjwa huo ipasavyo.
Akizungumza na Mzawa Online katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba iliyopo Manispaa ya Bukoba amesema Kagera ni Mkoa wa tatu kuongoza kwa maambukizi ya malaria nchini ambapo mwaka 2023 Halmashauri ya Ngara iliyoongoza kwa kiwango kikubwa cha maambukizi ambayo ilikuwa na asilimia 49%, ikafuatia Bukoba DC asilimia 41% .
Aidha Dkt Carlos amesema Halmashauri Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba imejitahidi kuwa na asilimia ndogo ya maambukizi ya ugonjwa huo na kwa mwaka huu kwa takwimu za Januari na aprili zinaonesha maambukizi yanaendelea kupungua kidogo japo Ngara inaendelea kuongoza kati Halmashauri zenye maambukizi.
Dkt Carlos amesema sababu walizozibaini zinazoendelea kuchochea maambukizi ni pamoja na matumizi yasiyo sahihi ya vyandarua vyenye dawa , wagonjwa kuchelewa kufika vituo vya kutolea huduma za tiba, mvua nyingi inayonyesha kwa misimu miwili kwa muda mrefu nakupelekea maji kutuwama maeneo mengi nakusababisha kuzaliana kwa mbu wa ambukizao malaria aina ya Anopheles.
Aidha Dkt Carlos amesema wanaendelea kuhamashisha jamii kuzingatia hatua mbalimbali kutoka kwa watalaamu wa afya hususani matumizi ya vyandarua, kuteketeza mazalia ya mbu kwakufukia mashimo yanyekutuwama maji, kufyeka nyasi, kuchoma chupa, kufika mapema Hopispitalini wanapohisi kuumwa, kutoa elimu kwa wajawazito ili kuwahi na kuhudhuria Kliniki kupewa dawa za “SP”matumizi sahihi ya dawa ikiwa ni sambamba na kufanya vipimo kabla ya kutumia dawa.
Dkt Carlos amesema Malaria ipo ya aina mbili ipo kali na isiyo kali, malaria kali dalili zake ni kuumwa kichwa, viongo vya mwili kuuma, kukosa hamu ya kula, tumbo kuuma, kuharisha na kutapika.
Malaria kali dalili zake ni degedege, kutapika kila kitu, mwili kuishiwa nguvu kusiko kawaida na kuchanganyikiwa pia ni ugonjwa ambao umekuwa ukiwaathiri pakubwa watoto na wajawazito.
Vilevile Dkt Carlos amewashukuru wadau wote wanaounga juhudi za kupambana na ugonjwa huo kwa Mkoa wa Kagera.
Hata hivyo Dkt Carlos amesema lengo la serikali ni kuhakikisha malaria inabakia “0” ifikapo 2030 kwani inawezekana iwapo kila mmoja atawajibika kuutokomeza.
Aidha Dkt Carlos Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuzingatia maelekezo wanayopewa na watalaamu wa afya badala yakuyapuuza kwani malaria ni miongoni mwa magonjwa hatarishi huku akiwahimiza watalaamu wa afya ngazi ya jamii kuendelea kuwafikia wananchi na kuwapa elimu kama ilivyokusudiwa na serikali.