Na Mwandishi Wetu.
Oktoba , 09 , 2024 – Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo, imeshirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC) ili kurahisisha ununuzi wa tiketi za Treni ya Mwendo Kasi (SGR) kupitia TigoPesa App.
Ushirikiano huu unalenga kurahisisha huduma kwa wateja kwa kuwawezesha kununua tiketi kwa njia ya kidijitali bila ya kufika kwenye vituo vya tiketi, hivyo kuboresha urahisi na ufanisi katika usafiri wa reli.
Akizungumza leo hii katika Ukumbi wa Stesheni ya Dar Es Salaam wakati wakiadhimisha wiki ya huduma kwa wateja na kumbukumbu miaka 30 tangu kuanza kutoa huduma Tanzania, Afisa Mkuu wa Tigo Pesa Bi. Angelica Pesha amesema, dhamira yao ni kuendelea kuwapa huduma bora wateja wao kwa wakati wote.
” Leo, tunajivunia kutangaza mfumo wa kisasa wa ulipaji wa tiketi za Reli ya Kisasa (SGR) kwa njia ya kidijitali, unaowezeshwa na Tigo Pesa. Ushirikiano huu kati ya Tigo na Shirika la Reli Tanzania (TRC) unaonesha dhamira yetu endelevu ya kurahisisha shughuli za kila siku na kuboresha uzoefu kwa wateja. Kupitia maboresho haya, abiria sasa wataweza kukata na kulipia tiketi za SGR kwa urahisi kwa kutumia simu zao, bila foleni ndefu. Hii ni kuhusu urahisi, ufanisi, na kuhakikisha kuwa kila msafiri anapata safari yenye utulivu na isiyo na usumbufu.
Ubunifu huu unaongozwa na azma yetu ya kujenga ushirikishwaji wa kifedha kwa Watanzania. Tigo Pesa haijawahi kuwa tu mfumo wa miamala ya kifedha bali ni mfumo kamili wa kifedha ulio jumuishi kwa mamilioni ya Watanzania. Kupitia huduma kama vile Nivushe Plus, ambayo inatoa mikopo midogo papo hapo, Kibubu Plus, inayowezesha kuweka akiba mara moja, Kikoba, inayowawezesha watu kuchangia fedha pamoja, na Lipa Ada, inayorahisisha malipo ya ada za shule,huduma hizi ikiwa kama ushahidi ya kwamba tunatatua changamoto za kila siku za wateja wetu. Huduma hizi husaidia watu kuokoa muda, kusimamia fedha zao, na kuwapa fursa ya kufanya shughli zingine ambazo wasingepata muda wa kuzifanya.
Kupitia huduma hizi za kifedha za kidijitali, hatubadilishi tu maisha ya watu binafsi bali pia tunaiwezesha jamii nzima. Kwa kutoa huduma hizi kwa wale ambao hawakuhudumiwa ipasavyo, tunajenga uchumi jumuishi zaidi. Ushirikishwaji wa kifedha ni nguzo muhimu ya mkakati wetu, na tunaamini kila mtu, bila kujali anapotoka au kipato chake, anapaswa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.
Huduma hii ya kidijitali ya ulipaji tiketi za SGR kupitia Tigo Pesa ni mfano bora wa jinsi ushirikiano kati ya sekta binafsi na ya umma unavyoweza kuleta mabadiliko makubwa. Kwa kushirikiana na TRC, tumeonesha jinsi ubunifu unavyoweza kuziba pengo, kuboresha huduma za umma, na kuleta thamani halisi kwa maisha ya kila siku ya Watanzania. Tunaamini kuwa ushirikiano ndiyo ufunguo wa maendeleo ya kitaifa. Ushirikiano kama huu kati ya sekta ya umma na binafsi unasaidia kufungua uwezo wa Tanzania na kutoa suluhisho zenye athari kubwa kwa jamii “.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TRC Bw. Masanja Kadogosa ameupongeza mtandao wa Tigo kwa hatua hii muhimu waliyoichukua kwa kurahisisha ukataji wa Tiketi kwa watanzania .
Husna Manyeki,Mteja wa TigoPesa Mkoa wa Iringa alisema yeye ni mteja wa TigoPesa tangu miaka ya nyuma hivyo alishukuru Tigo kwa kuendelea kutoa huduma bora na kuwasihi watu wote kutumia huduma za Tigopesa kwani ni rahisi na ni bora zaidi.
Huduma kwa wateja mwaka huu imeenda sambamba na kaulimbiu isemayo ‘Above & Beyond ‘ ambayo inathibitisha kwamba Tigo wako sako kwa bako na wateja wake.