Na Mariam Muhando- Dar es salaam.
Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam imetangaza fursa kwa Wawekezaji Nchini kuwekeza katika maeneo kumi na Moja ya Jiji hilo ili kupanua Wigo wa Mapato Jijini humo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Augost 11, 2024 jijini humo Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Jomaary Satura amesema ni sehemu ya mkakati wa Jiji hilo katika kupanua Wigo wa ukusanyaji wa Mapato.
Satura amebainisha maeneo hayo ni pamoja na eneo la Bibititi na Mkunguni plot namba 2451208 ambalo eneo hilo limependekezwa kuwa la maegesho ya Magari ya Uhakika.
“Eneo hili la Bibititi tunapendekeza tujenge Jengo kubwa la kitega uchumi Kwa ajili ya maegesho ya Magari kwani Jiji hili halina maeneo makubwa ya maegesho hivyo eneo hilo linastahili Uwekezaji,” amesema Satura.
Satura amesema kuna kiwanja namba 6 kitalu 12 eneo la Kisutu ambalo linafaa kwa ajili ya Uwekezaji wa Shopping Mall ambapo Uwekezaji huo utatatua changamoto ya Wananchi wanaofanya uchafuzi wa Barabara na mazingira kwenye eneo hilo.
“Tunalo eneo la Ufukwe lenye zaidi ya hekeri tisa ambalo tunatamani Wawekezaji waje kuwekeza Kwa ajili ya burudani ili Wananchi wa Dar er salaam waweze kupata burudani,” amesema Satura.
Amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha Halmashauri hio itatangaza rasmi kupitia Vyombo mbalimbali vya Habari ili kuwakaribisha Wananchi Kwa ajili ya Uwekezaji huo.
“Wawekezaji waje kuwekeza Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam sasa hivi inaongozwa kwa uwazi na uwajibikaji ili Kila mwenye uwezo wa kuwekeza ajitokeze kwa ajili ya ushindani,” amesema Satura
Nae Mstahiki Meya wa Jiji hilo Omary Kumbilamoto amemshkuru Rais Dr Samia Suluhu Hassani Kwa kufungua mianya ya Wawekezaji kuja kuwekeza hapa Nchini.
“Sisi kama Jiji tunayo maeneo takribani kumi na moja ambayo yametelekezwa na kusababisha kua msitu hivyo tunatarajia uwekezaji wenye tija na Wawekezaji ambao hawayafahamu maeneo hayo waje katika Ofisi zetu ili waweze kupewa maelekezo,” amesema Kumbilamoto
Wakati huo huo Kumbilamoto amewataka Wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika maeneo ya maegesho ya Magari wazingatie masuala ya zima moto ili kuepusha changamoto ya mlipuko wa moto kwenye maeneo hao.