Home Kitaifa JHPIEGO YATOA MSAADA WA VIFAA VYA AFYA MKOANI MARA KUKABILIANA NA VIFO...

JHPIEGO YATOA MSAADA WA VIFAA VYA AFYA MKOANI MARA KUKABILIANA NA VIFO VYA MAMA NA MTOTO

Na Shomari Binda-BUNDA

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Jhpiego kupitia mradi wake wa USAID Afya Yangu-Mama na Mtoto limetoa vifaa vya afya kukabiliana na vifo vya mama na mtoto.

Vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 38 vimekabidhiwa ofisi ya mkuu wa mkoa ambavyo vitapelekwa kwenye wilaya za mkoa wa Mara.

Akikabidhi vifaa hivyo mratibu wa mkoa wa mradi huo Erick Bakuza amesema vifaa vitakwenda kusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Amesema vifaa hivyo ambavyo ni vya maabara vya kupima damu kwa mama na vya usaidizi wa kupumua kwa watoto wanaozaliwa na changamoto hivyo vina umuhimu mkubwa.

Bakuza amesema vipo pia vifaa vya kujifunzia vyote vikiwa na lengo la kukabiliana na vifo vya mama na mtoto.

Amesema USAID Afya Yangu wamekuwa wakishirikiana na serikali katika masuala ya afya na kudai vifaa hivyo vinakwenda kuwa msaada kwenye eneo hilo la mama na mtoto.

Akipokea msaada wa vifaa hivyo kwenye kikao cha tathmini ya vifo vitokanavyo na uzazi kwa kipindi cha januari hadi machi kinachofanyika kwa siku 2 mjini Bunda Katibu Tawala wa mkoa wa Mara Gerald Kusaya amesema vifaa hivyo vimetolewa wakati muafaka.

Amesema wakati wataalamu hao wa afya mkoa wa Mara wanakutana kujadili namna ya kukabiliana na vifo hivyo vifaa vilivyotolewa vitakwenda kuwasaidia kwenye maeneo yao.

Kusaya ameshukuru shirika hilo kama mdau kwa vifaa walivyo vitoa na kuomba kufanyika kwa kipindi kingine huku akitoa wito kwa wadau wengine kushirikiana na serikali katika huduma za afya.

Katibu Tawala huyo wa mkoa wa Mara amewataka wataalamu wa afya kutumia kikao hicho kuja na mpango mzuri wa kukabiliana na vifo vya mama na mtoto.

Mganga mkuu wa mkoa wa Mara Dk.Zabron Masatu amesema katika kipindi cha januari hadi machi mwaka huu vifo 172 vya watoto na 15 vya mama vimetokea na wanakwenda kukaa na kuja na majibu ya kukabiliana navyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!