
Na Shomari Binda-Musoma
JESHI la Polisi mkoani Mara limetambua mchango wa mtoaji huduma za chakula Anifa Majura maarufu kama “mama Fugo” na kumpa cheti cha pongezi.
Cheti hicho cha pongezi amekabidhiwa na mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi katika hafla ya polisi family day iliyofanyika leo machi mosi kwenye viwanja vya Kikosi cha Kuzuia na Kutuliza Ghasia (FFU)
Akizungumza mara baada ya kupokea cheti hicho amesema anashukuru jeshi la polisi kwa kutambua mchango wake kama mjasiriamali na kumpa cheti hicho.
Amesema kupitia utoaji huduma za chakula na mapambo amekuwa na ushirikiano mzuri na jeshi la polisi katika kutoa huduma.
“Natoa shukrani kwa jeshi la polisi kwa kutambua mchango wetu nasi wajasiriamali na hii inatutia moyo wa kufanya kazi zaidi ya kutoa huduma.
“Tupo wengi tunaotoa huduma ya chakula na mapambo hivyo kutambuliwa mchango wangu nashukuru na niahidi kuendelea kushirikiana na jamii nzima na sio jeshi la polisi pekee“,amesema.
Akitoa tuzo kwa askari waliofanya vizuri katika kutimiza majukumu yao kwa mwaka 2024 na wadau waliotoa ushirikiano, mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi amesema kwenye suala la ulinzi na usalama mchango wa kila mmoja unatambuliwa.
Mtambi amewapongeza askari waliotimiza vyema majukumu yao na wadau ambao wametambuliwa michango yao kwa jeshi la polisi.
Hafla hiyo imehudhuriwa na maafisa wa jeshi la polisi,viongozi wa dini,familia za askari na wadau mbalimbali mkoani Mara..