Na Shomari Binda-Musoma
JESHI la Polisi mkoani Mara kupitia dawati la jinsia wanawake na watoto wilaya ya Musoma limefanikiwa kuwatoa watoto wa mtaani 26 na kuwarudisha majumbani.
Kazi hiyo imefanywa kwenye kipindi cha mwaka jana huku ikidaiwa wapo watoto ambao wengine walitoka nje ya mkoa wa Mara.
Hayo yamesemwa na mkuu wa dawati wilaya ya Musoma WP 4652 Sajenti Herieth Samson Tagatta alipokuwa akizugumza na Waandishi wa Habari kwenye wiki ya Sheria.
Amesema kwa mwaka jana wamezungumza na watoto 42 ambao waliwakuta mtaani wakizunguka zikiwemo nyakati za usiku na kuwaeleza wanapotoka.
Amesema baada ya kuelezwa wamezifatilia familia zao na kuongea nao na kufanikiwa kuwarudisha huku wengine wakiwa ni wa nje ya mkoa wa Mara.
Harierh amesema bado wanaendelea kufanya mawasiliano kwa kushiriiana na ofisi ya afisa maendeleo ya jamii ili watoto wengine waendelee kuunganishwa na familia zao.
Mkuu huyo wa dawati la polisi Musoma amesema watoto wengi waliopo mtaani wamechangiwa na migogoro kwenye familia na wapo wanaogoma kurudi nyumbani kutokana na migogoro hiyo na wengine kukwepa vipigo kutoka kwa wazazi wakambo.
Amesema ni jambo jema wazazi kutafuta usuluhishi inapoibuka migogoro ya kifamilia ili kuendelea kuwalea watoto kwa malezi ya baba na mama.
“Watoto wengi waliopo mtaani tuliozungumza nao ni migogoro ya kifamilia iliyowafanya kukimbia nyumbani na tuko hapa kwaajili ya kutoa elimu kwani Musoma bila watoto wa mitaani inawezekana”, amesema Harieth.