Home Kitaifa JESHI LA POLISI MARA LATAMBUA MCHANGO WA ASKARI NA WADAU KATIKA ULINZI...

JESHI LA POLISI MARA LATAMBUA MCHANGO WA ASKARI NA WADAU KATIKA ULINZI NA USALAMA

Na Shomari Binda – Musoma

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameongoza hafla ya Polisi Family Day ya mkoa wa Mara, iliyokwenda sambamba na utoaji wa tuzo kwa askari na wadau waliotoa mchango wao katika ulinzi na usalama.

Hafla hiyo imefanyika leo, Machi 1, katika viwanja vya Kikosi cha Kuzuia na Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Mara.

Katika hafla hiyo, askari waliofanya vizuri katika kutimiza majukumu yao ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao walikabidhiwa tuzo pamoja na kiasi cha shilingi laki tano.

Mbali na askari waliotunukiwa tuzo, wadau mbalimbali waliotoa mchango wao kwa Jeshi la Polisi mkoani Mara nao walitambuliwa kwa kupewa vyeti vya pongezi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, aliwapongeza askari waliofanya vizuri na kuwataka kuendelea kuzingatia maadili na kufuata maelekezo katika kutimiza majukumu yao.

Amesema maadili kwa askari ni jambo la msingi katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unadumishwa kwenye jamii.

Kwa upande wa wadau, amesema suala la usalama ni jukumu la kila mmoja, hivyo ni muhimu kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kudumisha usalama.

Niwapongeze sana askari na wadau ambao mchango wenu umetambuliwa katika suala zima la ulinzi na usalama wa raia na mali zao,” amesema.

Mmoja wa wadau waliotambuliwa kwa mchango wao, Anifa Majura, maarufu kwa jina la Mama Fugo, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kutambua mchango wake na ushirikiano wake na jeshi hilo.

Amesema kupitia huduma za chakula na mapambo, amekuwa na ushirikiano mzuri na Jeshi la Polisi kila anapohitajika.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi wa polisi, wadau wa usalama, viongozi wa dini, pamoja na familia za maafisa wa polisi na askari.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!