Home Kitaifa JESHI LA POLISI LAMOKOA MTOTO ALIYETEKWA, MTUHUMIWA AJERUHIWA KWA RISASI

JESHI LA POLISI LAMOKOA MTOTO ALIYETEKWA, MTUHUMIWA AJERUHIWA KWA RISASI

Na Magrethy Katengu – Mzawa Media
Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kumuokoa mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 8, mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbezi, Ubungo, aliyetekwa Machi 6, 2025, na Stanley Dismas Ulaya (18), mkazi wa Kata ya Nguruka, Wilaya ya Uvinza, Mkoa wa Kigoma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi, Jumanne Muliro, amesema kuwa Jeshi la Polisi lilimkamata mtuhumiwa Machi 8, 2025, lakini alipojaribu kutoroka akiwa chini ya ulinzi, askari walimpiga risasi ya tahadhari hewani bila mafanikio, hivyo ikalazimika kumpiga risasi mguuni na pajani. Kwa sasa mtuhumiwa yuko hospitalini chini ya uangalizi wa polisi akipatiwa matibabu.

MTOTO ALICHUKULIWA NJIANI KUELEKEA SHULENI

Kamanda Muliro ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea wakati mtoto aliposhuka katika daladala na kuelekea getini kuingia shuleni, ndipo mtuhumiwa alipomteka na kumpeleka katika eneo la vichaka Bagamoyo, mkoa wa Pwani. Mtuhumiwa alitumia namba ya simu ya mzazi aliyokuwa ameipata kwenye madaftari ya shule ya mtoto, akampigia na kudai kiasi cha shilingi milioni 50 ili kumuachia mtoto huyo, vinginevyo angemdhuru.

Mtuhumiwa alitumia vitisho vikali kwa mzazi, akimtaka atume fedha haraka la sivyo mtoto wake atauawa na maiti yake itupwe. Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilifanya ufuatiliaji wa kina na kufanikisha uokoaji wa mtoto akiwa salama,” amesema Kamanda Muliro.

MTUHUMIWA AKAMATWA, AJERUHIWA KWA RISASI

Kwa mujibu wa Kamanda Muliro, baada ya juhudi za ufuatiliaji, Jeshi la Polisi lilimkamata mtuhumiwa Machi 8, 2025, majira ya saa 1:00 usiku. Hata hivyo, alipofikishwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay, alijaribu kutoroka kwa kukimbia, hivyo askari wakalazimika kumpiga risasi mguuni na pajani baada ya tahadhari ya risasi za juu kutofua dafu. Hali yake imeripotiwa kuwa mbaya, na kwa sasa anapatiwa matibabu chini ya ulinzi mkali wa polisi.

MZAZI AMSHUKURU JESHI LA POLISI

Jonson Elisha, mzazi wa mtoto huyo, amesema kuwa alimpeleka mtoto wake shuleni asubuhi na kumuacha getini, lakini alipofika jioni mtoto hakurejea nyumbani. Alipojaribu kumtafuta shuleni, walimu walimweleza kuwa kuna namba ya simu isiyofahamika ilikuwa ikiwasumbua, na walimtaka awasiliane nayo.

Nilipopiga simu hiyo, mtu aliyepokea alidai kuwa nimtumie shilingi milioni 50 ili mtoto aachiliwe, vinginevyo nitakuta maiti yake. Nilichukua hatua za haraka kwenda kuripoti polisi kwa msaada,” amesema Jonson.

Jonson ameishukuru Jeshi la Polisi kwa juhudi zao, akisema kuwa Machi 8, 2025, alipigiwa simu kwenda kituo cha polisi kumchukua mtoto wake, ambaye alimkuta akiwa na afya njema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!