Na Shomari Binda
MAHAKAMA ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemtia hatiani mshitakiwa Alex Nangale mwenye umri wa miaka 24 mkazi wa mtaa wa Sokoni Wilayani Maswa kwa kujifanya askari polisi na kujipatia kipato.
Mshitakiwa huyo alishitakiwa katika Mahakama ya wilaya ya Mwaswa kwa shauri la jinai namba 45 la mwaka 2023 kwa makosa nane (8) kosa la kwanza likiwa ni kujifanya askari polisi kinyume na kifungu cha 369 (1) (2) na makosa saba yote ni kujipatia fedha kwa njia udanganyifu kinyume kifungu namba 302 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022 .
Awali Mahakamani hapo ilidaiwa na mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya taifa ya mashtaka wilaya ya Maswa Mkaguzi Msaidizi wa polisi Vedastus Wajanga kuwa mnamo tarehe 7/03//2023 katika mtaa wa Sokoni ndani ya wilaya ya Maswa mshitakiwa alijitambulisha Kwa Amos Malimi kuwa yeye ni askari polisi na yupo kituo cha polisi Maswa kitengo cha upelezi wa makosa ya jinai na kuanzia hiyo tarehe hadi tarehe 31/03/2023 alikuwa akiomba pesa kutoka kwa muhanga kwa kutumia utambulisho kuwa yeye ni askari polisi wa kituo cha polisi Maswa na yupo kitengo Cha upelelezi.
Taarifa zilifika kituo cha polisi ambapo mshtakiwa alikamatwa na kukiri kutenda makosa hayo na baada ya upelelezi kukamilika mshtakiwa alifikishwa Mahakamani
Jumla ya mashahidi wanne na vielelezo vinne vilitolewa na upande wa mashtaka na baada ya ushahidi huo mshtakiwa alijitetea .
Upande wa mashtaka uliomba mshitakiwa apewe adhabu kali ili iwe funzo kwake na kwa jamii kwani makosa ya watu kujifanya askari polisi au wataumishi wa serikali pamoja nakijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu yanaongezeka katika jamii na ukizingatia kuwa mshtakiwa ni kijana mwenye nguvu ambae anaweza kutafuta kipato chake halali .
Aidha upande huo mashtaka ulidai makosa kama hayo huchafua taswira ya taasisi husika na jamii inakosa imani na jeshi la polisi kwa tabia na vitendo alivyovifanya mshtakiwa
Mshtakiwa aliomba Mahakama impunguzie adhabu kwani ni mkosaji wa mara ya kwanza na ana familia inamtegea
Baada ya kusikiliza pande zote Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa Enos Misana hii leo mei 30 alimuhukumu adhabu ya kwenda jela miaka 5 kwa kosa la kwanza na miaka saba(7) kwa kosa la pili hadi la saba na fidia ya shilingi 1,174,000 kwa muhanga, adhabu zote zikienda kwa pamoja huku haki ya rufaa ikitolewa.