Na Theophilida Felician Kagera.
Wananchi Mkoani Kagera wahimizwa kula vyakula vya lishe bora kwa malengo kuutokomeza udumavu na utapiamlo kwa watoto na jamii kwa ujumla Mkoani humo.
Hayo yamebainishwa na Victoria Ngatunga Afisa lishe kutoka Hosptali ya Rufaa Bukoba akishiriki tamasha la Kagera Women Galla
lililofanyika Muleba.
Akiwasilisha mada ya lishe bora mbele ya akina mama walioshiriki tamasha hilo amesema kwamba lishe bora ni muhimu kwa kila mmoja hivyo yapaswa kila mtu awajibike kutimiza wajibu wakutumia vyakula vyenye lishe.
Ameeleza kuwa lishe bora iliyokamilika yatakiwa kula vyakula vyenye makundi matano baadhi yake ikiwa ni kundi la wanga kundi ambalo ni kitu kinachohitajika sana katika maisha ya mwanadamu, Protini, madini, na mboga mboga.
“Akina mama pia tunapaswa kufahamu maana ya lishe ili tuwe na afya bora hii itatusaidia zaidi licha yakufahamu kuwa udumavu kwa watoto umeongezaka lakini kuna magonjwa yasiyoambukiza yanayosababishwa na ukosefu walishe bora yakiwemo ya kisukari, saratani, presha na mengine” Victoria Matunga akifafanu.
Ameelimisha namna yakula vyakula hivyo vyenye makundi matano yaliyojumuisha nafaka, mizizi, maziwa, nyama, kunde, mboga mboga, mafuta na matunda.
Hata hivyo amedokeza kuwa mama mjamzito anapaswa kuhakikisha anakula vyakula vyote muhimu ili kumjengea afya bora mama na mtoto aliye tumboni hadi kuzaliwa na anyonyeshwe maziwa ya mama pekee kwamuda wa miezi sita.
Afisa huyo ametoa wito kwa jamii izingatie suala la lishe kwani hali ya udumavu na utapiamlo kwa Kagera bado ni changamoto kwa watoto.
Mkuu wa Mkoa Kagera Hajat Fatma Mwassa akiwa Mgeni rasmi katika tamasha hilo akitoa hotuba yake pia amezungumzia hali yakiwango cha utapiamlo na udumavu kilivyo kikubwa kwa 36% hivyo ameshukuru wanaumoja wa wanawake hao kuja na mkakati thabiti wakuongeza nguvu zaidi katika mapambano ya kuutokomeza.