Na Shomari Binda-Musoma
JAJI wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Fahamu Mtulya amesisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi ili kujiepusha na magonjwa.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati akifungua ofisi ya timu ya Biashara United veteran iliyopo nje ya uwanja wa kumbukumbu ya Karume katika kuongeza ufanisi wa utendaji wa timu hiyo.
Amesema mazoezi yana umuhimu mkubwa kiafya na yanapaswa kuzingatiwa na kila mmoja na kile wanacho kifanya wanachama wa Biashara United veteran kinapaswa kuigwa.
Jaji Mtulya amesema serikali imekuwa ikihimiza suala la kufanya mazoezi ikitambua inamfanya mtu kuwa na afya bora na kuendelea kufanya shughuli za kiuchumi,
“Niwapongeze sana wanachama wa Biashara United veteran kwa kufungua ofisi hii ambayo licha ya kufanya mazoezi ni sehemu ya kukutana.
“Tuendelee kufanya mazoezi kama ambavyo serikali ya Dkt.Samia Suluhu Hassan imekuwa ikisisitiza kutokana na umuhimu wake”amesema
Amesema watumishi wa umma na wafanyabiashara wa taasisi binafsi wanapaswa kutenga muda wa kufanya mazoezi ili kuwa na afya bora.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Biashara United veteran Dommy Mkono amesema lengo la kuanzishwa kwa timu hiyo ni kufanya mazoezi baada ya kazi ili kuboresha afya.
Amesema ushauri uliotolewa na Jaji Mtulya watauzingatia kwa kuhakikisha suala la mazoezi linakuwa ni kipaumbele chao.
Naye Katibu mkuu wa timu hiyo Melvin Nashon amesema ofisi iliyofunguliwa itasaidia masuala ya utendaji na kuwafanya kuwa karibu zaidi
Baada ya ufunguzi huo ulichezwa mchezo maalum wa ufunguzi kati ya timu ya Mwenyekiti Dommy Mkono na ya Makamu Mwenyekiti Castor Thomas ambapo timu ya makamu Mwenyekiti imeshinda mabao 2-0