Na Shomari Binda-Musoma
VIJANA wachezaji wametakiwa kuwa wa kwanza kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili jamii iweze kuishi salama na kushiriki shughuli za kiuchumi
Ujumbe huo umetolewa leo agosti 27 na Mkaguzi wa Polisi na askari Kata wa Kata ya Bweri Moses Mwaulambo kwenye muendelezo wa mashindano ya Polisi Jamii Cup Wilaya ya Musoma
Akizungumza na wachezaji wa timu ya Bweri na Mara Sport Mwaulambo amesema mahala ambapo hakuna uhalifu shughuli za kiuchumi ikiwemo michezo ufanyika kwa ufanisi
Amesema michezo kwa sasa ni sehemu kubwa ya uchumi na wachezaji wengi wanajipatia kipato hivyo ni vyema kushiriki michezo huku taarifa za uhalifu na wahalifu zikitolewa.
Mwaulambo amesema wahalifu sio watu wazuri kwani wanaweza kufanya uhalifu wa wizi wa mali ambazo mwanamichezo amezitafuta hivyo ni vyema kumtolea taarifa.
” Tuko hapa kwaajili ya kushiriki michezo lakini tunapeana ujumbe wa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwenye maeneo yetu.
” Wahalifu sio watu wazuri kwani wanaweza kufanya wizi wa mali ambazo tunazipata kupitia michezo hivyo tuwe tayari kuwatolea taarifa”,amesema.
Aidha Mkaguzi huyo wa polisi amewakumbusha washiriki wa mashindano hayo kujiandaa kushiriki uboreshaji wa daftari la wapiga kura litakaloanza septemba 4 hadi 10 pamoja na uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi novemba mwaka huu.
Katika mchezo wa leo timu ya Mara Sport imeitupa nje timu ya Bweri kwa kuifunga mabao 2-1 ambapo kesho ni mchezo kati ya Ajax na Buhare.