Na Magrethy Katengu
Shirika la bahari duniani [IMO] limeendesha warsha ya mafunzo ya siku 5 kwa taasisi zaidi ya 20 zilizopo Tanzania bara na Visiwani Zanzibar zinazohusika na masuala ya bahari ambayo ni utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo ya ulinzi wa bandari na uendeshaji salama wa vyombo majini.
Akizungumza wakati wa ufungaji wa warsha hiyo ya siku tano iliyofanyika jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa idara ya usalama na Mazingira kutoka wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Sekta ya Uchukuzi Stella Katondo amesema mafunzo hayo ambayo ni utekelezaji wa Mradi wa Usalama unaoratibiwa na IMO kwa kuishirikiana na wadau wengine.
Amesema mafunzo hayo ya siku tano yatasaidia kuleta weledi wa kukabiliana na vitendo viovu vinavyotendeka katika maeneo ya bahari ikiwemo uvuvi haramu,usafirishaji magendo kupitia bandari hivyo usalama na ulinzi wa bahari utadhibitiwa ipasavyo.
‘’Ili tutekeleze ile miongozo na mikataba ya shirika la bahari duniani ni lazima tuweze kuridhia kama nchi yetu kwa utaratibu wake wa kisheria tukisharidhia mkataba ni lazima kuweka namna ya utekelezaji katika sharia zetu ndiyo maana wizara kwa kushirikiana na IMO tupate uwezeshwaji kwani kuna mikataba mingi zaidi ya 50 kama nchi lazima tuangalie kipaumbele pamoja na kwamba yote inahusu usafirishaji salama wa bahari” amesema Mkurugenzi Katondo
Mafunzo hayo yalikutanisha watu kutoka taasisi mbalimbali zaidi ya 20 kutoka Tanzania bara na Visiwani Zanzibar zinazohusika katika kutekeleza masuala ya ulinzi wa bahari na usafiri salama wa vyombo baharini ambapo kutokana na umuhimu wa mafunzo hayo shirika la IMO limesema liko tayari kuendelea kutoa mafunzo hayo kupitia shirika la uwakala wa meli Tanzania[TASAC].
Kwa upande wake mkurugenzi wa huduma za sharia kutoka shirika la uwakala wa meli [TASAC], Judith Kakongwe amesema warsha hiyo ya kitaifa itasaidia katika masuala ya ulinzi wa bahari kwa taasisi mbalimbali kwa kujua namna ya utekelezaji wa sharia zilizowekwa
Hata hivyo amesema shirika la uwakala wa meli Tanzania ndilo linalowajibika kusimamia utekelezaji wa sheria zilizopo na zinazoandaliwa katika usafiri wa maji nchini kwani hufanyika kuendana na miongozo kwa maana mikataba ya kimataifa ambapo kama mwanachama Tanzania imeridhia katika ulinzi na usalama wa bahari.
Aidha ameongeza kuwa Tanzania kama mwanachama wa IMO ni lazima mikataba iliyoridhia iwekwe kama sheria na itekelezwe na isimamiwe kwa watoa huduma za vyombo vya bahari vinapokuwa vinakuja kwenye maji ya Tanzania [bahari]iweze kufanywa kwa misingi iliyoelekezwa na shirika la bahari duniani.