Home Kitaifa ILEMELA YAKABIDHIWA MPANGO WA USIMAMIZI WA MAAFA

ILEMELA YAKABIDHIWA MPANGO WA USIMAMIZI WA MAAFA

NA. MWANDISHI WETU

SERIKALI imekabidhi nyaraka za usimamizi wa maafa katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Jijini Mwanza huku ikisisitiza kuwa, ni muhimu masuala hayo kujumuishwa katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku siku ili kuendelea kuwa na matokea chanya katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini.

Wito huo umetolewa Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala akimwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Nyaraka za Usimamizi wa Maafa katika halmashauri hiyo.

Nyaraka zilizokabidhiwa ni pamoja na za Matokeo ya tathmini ya vihatarishi, mpango wa kujiandaa na kukabiliana na maafa na mkakati wa kupunguza vihatarishi vya maafa nchini.
Amesema kuwa uandaaji wa nyaraka hizo za usimamizi wa maafa ni hatua nzuri kueleka katika ujenzi wa jamii iliyo stahimilivu dhidi ya majanga katika Manispaa ya Ilemela. Brigedia Jenerali Ndagala ametoa wito kwa Idara, Vitengo na Taasisi zote zilizopo katika Halmashauri hiyo kuzingatia dira hii katika kutekeleza vipaumbele vya kisekta.

“Nitoe wito kwamba, nyaraka hizi zilizoandaliwa ziwe ni chachu ya kuongeza ushirikishwaji wa jamii na wadau, kujenga uelewa wa jamii kuhusu masuala ya usimamizi wa maafa,kuimarisha mfumo wa utoaji tahadhari ya awali, kujenga uwezo wa kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa na maafa na kujenga uwezo wa kukabiliana na maafa.”alieleza

Amebainisha kuwa matokeo ya tathmini ya maafa iliyofanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mwezi Februari, 2024 yameonesha kuwa Manispaa hiyo imekuwa ikikabiliwa na maafa.

Ameeleza kuwa maafa hayo yamekuwa yakisababishwa na majanga ya mafuriko, upepo mkali, moto, magonjwa ya mlipuko pamoja na ajali za barabarani na majini.
Amesema anatambua kwa sasa Manispaa hiyo inakabiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu hivyo kuwapongeza kwa jitihada wanazoendelea nazo katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Aidha, amewasisitiza kuendelea kuchukua jitihada mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu.

“Ni imani yangu kuwa matokeo ya tathmini iliyofanyika yamezingatiwa ipasavyo katika kuandaa Mpango wa Kujiandaa na Kukabili Maafa na Mkakati wa Kupunguza Vihatarishi vya Maafa katika Manispaa ya Ilemela. Hivyo, ni matumaini yangu kuwa, mpango huu utasaidia sana kuongeza ufanisi katika kukabiliana na maafa kwa kuwa unaainisha majukumu ya wadau wote wanaohusika na masuala ya maafa katika Manispaa ya Ilelemela kabla, wakati na baada ya maafa kutokea. “amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masala ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kuratibu masuala ya maafa nchini huku akieleza kuwa, wamepokea nyaraka hizo za Usimamizi wa Maafa ili kuendelea kuwa na nguvu ya pamoja katika kukabiliana na maafa nchini.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa Wilaya itautumia kwa manufaa huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha jamii inakuwa stahimilivu katika masuala ya menejimenti ya maafa.

“Tutaendelea kutoa elimu kuhusu masuala haya ya maafa na kuhakikisha kamati yetu ya maafa inatekeleza kikamilifu majukumu kwa tija na matokeo yaliyokusudiwa,” alisema
=MWISHO=

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!