Na Ramadhani Kissimba na Farida Ramadhani, WF – Nairobi
Taasisi ya Fedha ya Kimataifa (International Finance Cooperation – IFC) imeishauri Tanzania kuchagua miradi mikubwa michache, endelevu na inayovutia uwekezaji katika Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) ili kufungua biashara na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Shaaban kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, baada ya kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkaazi wa Taasisi hiyo, Bi. Amena Arif, kando ya Mikutano ya Mwaka 2024 ya Bodi ya Magavana (Mawaziri wa Fedha kutoka nchi wanachama) wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Jijini Nairobi nchini Kenya.
Bi. Amina alisema wamekubaliana na Taasisi hiyo kukutana tena kwa ajili ya kuangalia miradi ya PPP ambayo ipo kwenye mchakato ili kuweza kuchagua miradi bora kwa maendeleo ya nchi na wananchi kwa ujumla.
“Ili tuweze kufanikiwa katika utekelezaji wa miradi ya PPP, IFC imeshauri tuchague miradi mikubwa kiasi ambayo ni endelevu na itavutia uwekezaji”, alibainisha Bi. Amina.
Alisema IFC imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ya uwekezaji ili kuhakikisha nchi inanufaika vyema na miradi itakayotekelezwa kupitia Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi.
“Kwa kuwa pia ni washauri, IFC imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya Ujenzi wa Miundombinu ya Mfumo wa Usafiri wa mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya Tatu na Nne”, alisema Bi.Amina.
Aidha Bi. Amina aliongeza kuwa katika kikao hicho Tanzania na Taasisi hiyo wamekubaliana kukaa pamoja ili kuainisha aina ya miradi ambayo itakuwa na tija kwa maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi wa Taasisi hiyo, Bi. Amena Arif alisema IFC inajivunia ushirikiano uliopo kati yao na Tanzania, kupitia ushirikiano huo IFC ina imani kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali utafanyika kwa wakati na ufanisi.
Bi. Arif aliongeza kuwa ushirikiano uliopo umewezesha utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka ambao unasimamiwa na Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (DART).
IFC ni Taasisi ya Fedha ya Kimataifa ambayo ni mwanachama wa kundi la Benki ya Dunia (Word Bank Group) inayotoa huduma za uwekezaji, ushauri na usimamizi wa miradi ili kuchochea maendeleo ya sekta binafsi katika nchi zinazoendelea.