Mkoa wa Geita umeendelea kusonga mbele kiuchumi kufuatia uzinduzi wa hoteli mpya ya Desire, iliyopo Manispaa ya Geita, ambayo inatarajiwa kuboresha huduma za kitalii, kuchangia ukuaji wa uchumi wa ndani, na kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, alieleza kuwa hoteli hiyo itatoa ajira kwa wakazi wa eneo hilo na kuuweka mkoa wa Geita kwenye ramani ya ushindani mkubwa katika sekta ya utalii na uwekezaji.
“Ufunguzi wa hoteli kama hizi ni kielelezo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa mkoa wetu. Tunakaribisha zaidi wawekezaji kuja Geita.” Martine Shigela – Mkuu wa Mkoa wa Geita:
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Desire, Saimon Rwehimamu, alisisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuwa na wivu wa maendeleo kwa kuwekeza kwenye miradi ambayo itachochea uchumi wa mkoa huo.
“Ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba uwekezaji tunaoufanya unaleta tija kwa jamii, hasa katika kuboresha maisha ya watu na kuongeza fursa za ajira.” Saimon Rwehimamu – Mfanyabiashara, Geita:
Aidha, Kiganga Bugomola, mfanyabiashara maarufu wa mkoa huo, aliunga mkono juhudi hizo akisema kuwa hatua kama hizo zitasaidia kubadilisha sura ya Geita.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Flavian Kasala, ambaye alihudhuria hafla hiyo, alitoa wito kwa serikali na wakazi wa Geita kuendelea kuboresha mji huo na kujiandaa kufikia hadhi ya kuwa jiji.
“Hatupaswi kuridhika na tulipo sasa. Lazima tuwe na ndoto kubwa ya kuubadilisha mji wetu kuwa jiji litakalovutia uwekezaji wa kiwango cha juu.” Askofu Flavian Kasala – Kanisa Katoliki Jimbo la Geita:
Uzinduzi huu ni ishara ya nafasi kubwa inayosubiriwa kutumika katika sekta ya utalii na miundombinu ndani ya Geita. Kwa kushirikiana kati ya sekta binafsi na serikali, mkoa unazidi kuwa sehemu ya kupigiwa mfano kwa maendeleo na uwekezaji.