Na Magrethy Katengu-Dar es salaam
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amezitaka hospitali nchini kuboresha huduma zao kwa kufanya miadi ya wagonjwa ya kuwaona madaktari kupitia mifumo ya TEHAMA.
Dkt. Jungu ametoa kauli hiyo Mei, 16 ,2024 jijini Dar es Salaam akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ziara ya kukagua huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa Mkoa Amana na utekelezaji wa miradi.
Ameeleza kuwa wagonjwa wanatakiwa kutumia mifumo hiyo kuweka miadi ya kupatiwa matibabu na kupangiwa siku na muda wa kumuona daktari husika na kupatiwa matibabu jambo ambalo litasaidia na kurahisisha kuimarisha kutoa huduma kwa wagonjwa pamoja na kuepuka kupoteza muda.
“Mtu kokote aliko awe anatoka Dar es Salaam ama mkoani basi atalazimika kupiga simu au kutumia mifumo ya barua pepe na mingine itakayowekwa kuomba kufika hospitalini hapa kutibiwa bila kujali simu ni ya kisasa au kitochi mfumo huo utawafikia,” amesema Dkt. Jingu.
Wakati huohuo Dk. Kingu ameweza kuwakabidhi hati ya umiliki wa ardhi Hospitali hiyo yenye ukubwa wa hekari sita ambapo awali walikuwa wakiendesha shughuli za matibabu bila kuwa na hati miliki.
Kwa upande wake Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Amana Dkt. Bryceson Kiwelu amesema kuwa agizo hilo la Katibu Mkuu wamelipokea kwa mikono miwili kwani walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya msongamano wa wagonjwa na malamamiko mengi kutoka kwa wagonjwa kutokana na kila mmoja kutaka kutibiwa kwa wakati.
Amesema wanajipanga kuanza kutoa elimu kwa wananchi na wagonjwa kuhusiana na matumizi ya teknolojia hiyo ya kutumia mifumo hiyo kabla ya kuanza kwa kutumia rasmi ili kuondoa sintofahamu kwa wagonjwa.
Amesema mfumo wa Tehama ulianza mwaka 2012 kwa kuwahudumia wagonjwa kwa kupatiwa majibu na huduma zingine lakini bila kutumia kwa kufanya miada kufika hapo ambapo wanajipanga kuanza muda si mrefu kutokana na gizo hilo.
“Mfumo huo utatusaidia kwa kiwango kikubwa kwani kinachotokea sasa hivi wagonjwa wote wanafika kwa wakati mmoja na kila mmoja ana ona yeye muhimu kupatiwa huduma kuliko mwingine” amesema Dk. Kiwelu.
Amesema wastani wa kupokea wagonjwa hospitalini hapo ni wagonjwa 650 hadi 700 kwa siku ambapo idadi hiyo imepungua toka kutokea kwa janga la Covid-19 ambapo awali walikuwa wakipokea wagonjwa 1000 na zaidi kuja kupata matibabu hospitalini hapo.
Aidha ziara hiyo iliweza kutembelea miradi ya hospitali hiyo ikiwemo kuona mtambo mpya wa kuchomea taka ambao utakuwa mradi wa kuingiza mapato ya ndani ambapo wataweza kupokea taka toka katika hospitali zingine na wataweza kuwahudumia huduma hiyo kwa kuwachomea kwa Shilingi elfu tano kwa kilo moja.