Na Shomari Binda – Musoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imesema hospital ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo mkoani Mara imetengwa kuwa hospital inayotoa huduma za kibingwa magonjwa ya mifupa na misuli.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alipotembelea hospital hiyo pamoja na mambo mengine kuangalia huduma zinazotolewa.
Amesema serikali katika bajeti yake ya mwaka 2024/2025 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 13 kuendeleza ujenzi wa hospital hiyo.
Waziri Ummy amesema moja ya muendelezo huo ni kuwa na kitengo cha utoaji huduma za kibingwa za magonjwa ya mifupa na misuli kwenye hospital hiyo.
Amesema hospital hiyo kwa eneo la kanda ya ziwa itakuwa ni hospital pekee inayotoa huduma hiyo ili kuweza kuwasaidia wananchi.
Waziri Ummy amesema tayari madaktari kutoka hospital ya taifa Muhimbili kitengo cha mifupa (MOI) wametumwa kufanya utafiti kwenye hospital hiyo.
Amesema katika kiasi hicho cha fedha kilichotengwa zipo za uendelezaji ujenzi wa wodi ya watoto wa wachanga kuanzia siku 0 hadi 28 na wale wanaozaliwa na changamoto.
Amesema lengo la ujenzi wa wodi hiyo ni kuhakikisha kila mtoto anayezaliwa anaishi kwa kupatiwa huduma stahiki katika siku za awali baada ya kuzaliwa.
Aidha Waziri Ummy amesema ameridhia kutolewa hekari 20 kwaajili ya ujenzi wa chuo cha Tiba kitivo cha chuo kikuu cha kilimo na teknolojia cha Mwalimu Nyerere(MJMNUAT)
Baadhi ya wananchi waliokuwepo hospitalini hapo wameishukuru serikali kwa kuendeleza ujenzi wa hospital hiyo na kuomba kutolewa huduma ya X-Rey na uboreshaji wa barabara.
Mkuu wa mkoa wa Mara Said Mtanda amesema serikali itafanya ujenzi wa kipande cha barabara kuweza kufika kwa urahisi kwenye hospital hiyo