Home Kitaifa HESLB YAANZA KUWADAI TZS BILIONI 10.6 WALIOKOPESHWA ‘Law School of Tanzania’

HESLB YAANZA KUWADAI TZS BILIONI 10.6 WALIOKOPESHWA ‘Law School of Tanzania’

Wanasheria 5,065 waliokopeshwa zaidi ya TZS 10.6 bilioni kama mikopo wakiwa wanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria Tanzania (Law School of Tanzania – LST) sasa watapaswa kurejesha mikopo hiyo kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Wanasheria hawa ni wale walionufaika na mikopo ya elimu wakiwa wanafunzi wa LST kati ya mwaka 2008 na 2015 wakisoma Stashahada ya Juu ya Uanasheria kwa Vitendo (Post Graduate Diploma in Legal Practice) wakati Sheria ya HESLB ilipokua hairuhusu wanafunzi wa LST kukopeshwa. Sheria ya HESLB ilirekebishwa mwaka 2014 na kuruhusu wanafunzi wa LST kukopeshwa na HESLB.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa jijini Dar es salaam leo (Jumanne, Juni 21, 2022) na Watendaji Wakuu wa taasisi hizo, wanasheria hao ni wale waliosoma kupitia kundi (cohort) la kwanza hadi 19 na kukopeshwa na Serikali kupitia LST.

“Tunashukuru kuwa mikataba waliyosaini walipokua wanafunzi-wanasheria ipo wazi kuwa LST inaweza kuipa kazi ya kukusanya madeni haya taasisi yoyote ya umma au binafsi … na hivyo baada ya mazungumzo tangu 2019, leo tumefikia hatua hii,” amesema Jaji Dkt. Benhajj Masoud, Mkuu wa LST katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema HESLB ina uzoefu na utayari wa kutekeleza jukumu hilo na kuwakumbusha wanufaika hao kujitokeza na kurejesha.

“Tumejipanga kuanza kuwahudumia kuanzia Julai 1, 2022 … hivyo tunatoa wito kwa wateja wetu hawa kurejesha fedha hizi pamoja na zile walizokopeshwa wakiwa wanafunzi wa shahada za kwanza ili ziwanufaishe vijana wengine wa kitanzania wanaohitaji,” amesema Badru.

HESLB ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa na majukumu makuu mawili, kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji wa elimu ya juu na pia kukusanya fedha za mikopo zilizoiva ambazo zimezotolewa na Serikali kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu tangu mwaka 1994/1995.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!