Na Shomari Binda- Musoma
HATUA ya makundi ya mashindano ya Mathayo Cup 2023 itafikia tamati kesho kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Ufundi Musoma.
Michezo ya kesho itaziikutanisha timu za kundi D ambapo kwenye mchezo wa mapema majira ya saa 8 mchana timu ya Nyakato itaikaribisha timu ya Rwamlimi huku majira ya saa 10 Bweri fc wakiwa wageni wa Mshikamano.
Katika kundi hilo kesho pia zitafahamika timu 2 zitakazoungana na nyingine 6 kutinga hatua ya robo fainali.
Timu nyingi 6 ambazo tayari zimeingia robo fainali ni Kitaji fc, Mwigobero fc, Makoko fc na Mwisenge fc, Nyasho fc na Nyamatare fc.
Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano wa timu ya Nyasho, Juma la Familia amesema hatua ngumu ilikuwa ya makundi na baada ya kupita wanakwenda kutetea ubingwa wao.
Amesema licha ya timu nyingi kuikazia kwenye michezo yao lakini wanapambana kuendelea kufanya vizuri.
Kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Nyakato, kocha wa Rwamlimi, Abdara Hamid” Dulla” amesema licha ya kutokufanya vizuri kwenye michezo miwili iliyopita kesho wanakwenda kupata matokeo mazuri.
Amesema mchezo wa kesho ni wa kufa na kupona ili kuweza kupata matokeo mazuri ili kupata nafasi ya kutinga robo fainali.
Mmoja wa warayibu wa mashindano hayo,Marwa Matiko,amewataka wachezaji wa timu zote kuendelea kudumisha nidhamu na kuwa na kujenga umoja na mahusiano kupitia mashindano hayo.