Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeibuka kinara kati ya halmashauri sita za Mkoa wa Geita katika matokeo ya Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika Oktoba 5, 2024.
Mbio hizo zilianza rasmi Mkoani Kilimanjaro tarehe 2 Aprili 2024, ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa (MB), alizindua mbio hizo. Mwenge wa Uhuru ulikamilisha mbio zake jijini Mwanza tarehe 14 Oktoba 2024, kwenye hafla iliyohitimishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali cha Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ndg. Alex Herman, alieleza furaha yake kwa matokeo hayo, akisema kuwa haikuwa kazi rahisi.
“Sikutegemea, kwa kweli, kutokana na changamoto nyingi wakati wa maandalizi, lakini Mwenyezi Mungu ametuwezesha na hatimaye tumekuwa washindi,” alisema Alex.
Aidha, Mratibu huyo alitoa shukrani zake kwa kamati zote zilizohusika katika maandalizi na mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2024, akiwashukuru kwa namna ya kipekee kamati ya ulinzi na usalama ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Mh. Hashim Komba, Mkurugenzi Ndg. Karia Rajabu Magaro, viongozi wa chama na dini, wakuu wa idara na vitengo, pamoja na wananchi wote kwa ushirikiano wao.
Pamoja na kuwa ya kwanza kimkoa, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeshika nafasi ya 6 kwa Kanda kati ya halmashauri 45 na kushika nafasi ya 17 kitaifa kati ya halmashauri 195 zilizokimbiza Mwenge wa Uhuru 2024.
Mwenge wa Uhuru ni chombo kilichoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka 1961 ikiwa ni ishara ya uhuru wa Tanganyika. Mbio za Mwenge wa Uhuru zilianza rasmi mwaka 1964 baada ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar, hatua iliyozalisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwenge wa Uhuru umekuwa na mchango mkubwa katika kudumisha uhuru, umoja wa kitaifa, amani, Muungano wa Tanzania, na kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii ndani na nje ya nchi.
Mwisho.