Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan amewataka Walipakodi nchini kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kuacha vitendo vya ukwepaji Kodi ambavyo vinaondoa usawa wa ushindani sokoni.
Akizungumza wakati wa utolewaji wa Tuzo za Mlipakodi January 23, Jijini Dar es Salaam Rais Dk. Samia amesema utolewaji wa tuzo hizo unachochea ulipaji wa Kodi kwa hiari na kuwataka wenye tabia za kukwepa kodi kuacha mara moja kwani wanadhoofisha Uchumi wa Nchi na kuwavunja moyo Walipakodi waaminifu kwa kuweka ushindani usiokuwa sawa sokoni.
Rais Samia ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao ndiyo wameandaa tuzo hizo kuendelea kupambana na watu wanaokwepa Kodi kwa kuwasaka wanaoghushi risiti za EFD na VFD pamoja na wanaotumia Stempu bandia kwenye vinywaji.
“Dhuluma siyo kitu kizuri hivyo wanaokwepa Kodi watambue kuwa wanafanya dhuluma Hali kadhalika watumishi wa TRA wanaofanya makadirio yasiyokuwa sahihi nao wanafanya dhuluma, tuache” Dk. Samia.
Dk. Samia amesema mwelekeo wa Serikali ni kuongeza idadi ya Walipakodi na siyo kuwatumia wachache waliopo na Hali hii itafanikishwa na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iwe rasmi na kulipa Kodi kikamilifu.
Rais Samia amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM inaitaka Nchi ipunguze utegemezi na utegemezi huo utapungua kwa kusimamia kwa usahihi ukusanyaji wa Kodi jambo ambalo litaifanya Tanzania ijiamini.
Rais Samia amesema Bajeti ya Serikali ni Sh. Trilion 49.34 na miongoni mwa fedha hizo Sh. Trilion 30.4 sawa na asilimia 61.6 inatokana na makusanyo ya Kodi kutoka kwa TRA hiyo ndiyo inaonyesha tunavyouendea kujitegemea hivyo ongezeni juhudi katika kukusanya Kodi.
Rais Samia amesema Mwaka ujao 2025/2026 hakutakuwa na Tuzo za Mlipakodi za TRA bali kutakuwa na Tuzo za Rais ili kuonyesha umuhimu wa kulipa Kodi.
“Kwenye masuala ya Kodi hakuna mzaha, mtu asijifanye kwamba ana maelekezo kutoka juu asilipe Kodi, napenda kuwaambia hakuna mtu yoyote niliyemruhusu asilipe Kodi na Mimi ndiyo ngazi ya juu ya mwisho, kama nitamruhusu mtu yoyote nitatoa maagizo kwa barua” Rais Samia
Kuhusu masuala ya kesi za kikodi ameitaka Bodi ya rufani kuharakisha usikilizaji wa kesi hizo ili Kila mmoja apate haki yake.
Rais Samia ametoa rai kwa watumishi wa TRA kufanya kazi kwa uaminifu, kudumisha nidhamu kwa kuwa na mienendo mizuri kazini ili kuwajengea Imani Walipakodi.