Wakuu wa Mikoa na Wilaya waendelea kuvipokea Vitabu vya Madini
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeendelea kutekekeza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kusambaza Vitabu vinavyoonesha Madini yapatikanayo Tanzania kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini alilolitoa katika Kongamano la Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA).
Katika kutekekeza agizo hilo, leo Septemba 20, 2023 GST imewasilisha nakala ya Kitabu kipya toleo la Tano la Mwaka 2023 kilichoandaliwa na taasisi hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya.
Malenya ameipongeza GST kwa kuona umuhimu wa kuandaa kitabu hicho ambacho kitasaidia Wilaya, Mikoa na Taifa kwa ujumla na kuchochea uwekezaji katika Sekta ya Madini kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Sambamba na hayo, Malenya ametumia fursa hiyo kutoa mwaliko kwa GST kushiriki Mdahalo wa Wadau kuhusu Fursa za Uwekezaji Wilaya ya Namtumbo utakaofanyika katika ukumbi wa St. Agness-Namtumbo Septemba 21, 2023 Wilayani Namtumbo Mkoa wa Ruvuma ambapo mada mbalimbali na fursa zilizopo mkoani humo zitajadiliwa katika Kongamano hilo.
Kwa upande wake, Meneja wa Sehemu ya Jiolojia kutoka GST Maswi Solomon amesema, mbali na madini mengine, Mkoa wa Ruvuma hususan Wilaya ya Namtumbo imebahatika kuwa na madini ya Urani ambayo ni miongoni mwa Madini Mkakati yanayohitajika kwa wingi kwenye nishati safi (clean energy) ili kuondokana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na hewa ya ukaa
Pamoja na Mambo mengine, Maswi amesema jukumu kubwa la GST ni pamoja na kufanya tafiti, kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusiana na madini na kuratibu majanga ya asili ya jiolojia ikiwemo elimu ya aina ya miamba inayoweza kuzalisha mionzi na sumu kwa mazingira.