GST yashiriki Kongamano la Wadau kuhusu Fursa za Uwekezaji Namtumbo
Wilaya ya Namtumbo imetajwa kuwa na fursa kubwa ya uwepo wa Utalii wa Madini baada ya kugundulika kuwa na kiasi kikubwa cha madini ya Urani ambapo ndiyo utakuwa na mgodi wa kwanza wa uzalishaji wa Madini hayo kwa Afrika Mashariki na miongoni mwa nchi chache zitakazo kuwa na mgodi wa urani duniani.
Hayo ameyabainisha Meneja wa Sehemu ya Jiolojia Maswi Solomon wakati akimuwakilisha Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kutoa mada kwenye Kongamano la Wadau kuhusu Fursa za Uwekezaji Wilaya ya Namtumbo lililofanyika katika ukumbi wa St. Agness-Namtumbo uliopo Wilayani humo.
“Mgodi wa kuzalisha Urani wa Mkuju ndiyo utakuwa mgodi wa kwanza Afrika Mashariki kuzalisha Urani, hivyo tunaona ni fursa kwetu katika kuchochea Utalii wa Madini kwa watu kuja kujionea ni namna gani kama nchi tumeweza kuendesha mgoni wa Urani unaoweza kutoa mionzi yenye madhara kama tahadhari isipozingatiwa, hivyo Wilaya ya Namtumbo inaenda kuwa kitovu cha Utalii wa Madini na mtapokea wageni wengi kuja kujifunza uzalishaji wa madini hayo kama ambavyo na sisi tumekuwa tukienda kujifunza kwenye migodi ya nchi kama Namibia,” amesema Maswi.
Maswi amesema GST inajukumu kubwa la kukusanya taarifa za madini kwa ajili ya kuchochea uwekezaji na kuishauri Serekali lakini pia, ina jukumu la kutoa elimu ya majanga ya asili ya Jiolojia ikiwemo matetemeko ya ardhi na madhara ya Jiolojia kama milipuko ya volkano na miamba inayoweza kuwa na sumu au mionzi.
Pia, Maswi amesema Namtumbo imebahatika kuwa na madini ya Urani ambayo yanatumika kutengeneza nishati safi isiyo na hewa ya ukaa na amewatoa wasiwasi wakazi wa Namtumbo kuwa, uchimbaji wa madini ya Urani hauwezi kuathiri mazingira kama taratibu za kitaalamu zitazingatiwa katika uchimbaji na uchakataji wake ambapo ametoa mfano kwa nchi za Namibia, Niger, Afrika Kusini na Gaboni ambapo uzalishaji wake unaendelea lakini hakuna madhara yoyote yaliyotokea hivyo Tanzania haita kuwa nchi ya kwanza kuwa na mgodi wa Urani kwa Afrika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Ngollo Malenya amefarijika kuona Wilaya ya Namtumbo kuwa na madini ya aina mbalimbali ikiwemo urani, dhahabu, chuma, Ulanga na Vito mbalimbali ambapo Kampuni ya Mantra imejenga mgodi mdogo wa majaribio kwa ajili ya kuanza kuyavuna madini hayo.
“Kama tungepata Wawekezaji wengi, Wilaya ya Namtumbo tungekuwa mbali kimaendekeo hivyo, kupitia Kongamano hili naomba tushirikiane ili tuone ni kwa namna gani tutaweza kuinua Sekta ya Madini katika Wilaya yetu,” amesema Malenya.
Kongamano hilo lililokutanisha zaidi ya washiriki 400 limebebwa na Kauli Mbiu isemayo “Mapinduzi ya Kilimo, Biashara Utalii Hifadhi ya Mwalimu Nyerere na Utalii wa Madini”.