Geita,Tanzania
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita limekutana kujadili na kupitisha mpango wa wajibu wa Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) kwa jamii (CSR) kwa mwaka 2024, unaolenga kutekeleza miradi ya maendeleo wilayani humo.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Nzera, na kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa GGML, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Geita, na wataalamu wa halmashauri.
Kwa miaka mitano mfululizo, Halmashauri ya Geita imekuwa ikiingia mkataba wa utekelezaji wa miradi ya CSR na GGML, ambapo kila mwaka kampuni hiyo inachangia Shilingi Bilioni 4.3 kwa ajili ya maendeleo ya jamii. Mpango huu ni kwa mujibu wa kanuni ya kifungu Na. 4-(1) ya mwongozo wa mwaka 2023, inayomtaka mmiliki wa leseni ya madini kuandaa mpango wa wajibu wake kwa jamii inayozunguka shughuli zake za uchimbaji.
Katika kikao hicho, baadhi ya madiwani walihoji kuhusu kutokamilika kwa miradi ya maendeleo iliyokuwa imepangwa kupitia mpango wa CSR wa mwaka 2021-2023. Walisema kucheleweshwa kwa miradi hiyo kumewanyima wananchi fursa ya kunufaika na huduma zinazopaswa kutolewa. Sababu zilizotajwa ni pamoja na ucheleweshwaji wa michakato ya manunuzi, fedha za miradi kutokuwa halisi, na wazabuni kushindwa kutoa vifaa kwa wakati.
Mbunge wa Geita, Mhe. Dkt. Joseph Kasheku Msukuma, alikosoa uongozi wa mgodi huo kwa kutokamilisha miradi kwa wakati na kuwataka kuzingatia makubaliano ya mkataba (MoU) ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kama ilivyopangwa. Alisema, “Msiwe chanzo cha kukwamisha miradi ya maendeleo kwa kutoa taarifa zisizo sahihi kwa viongozi wenu.”
Mbunge wa Busanda, Mhe. Mhandisi Tumaini Magesa, alisisitiza umuhimu wa GGML kuzingatia vijiji vinavyohusishwa na miradi yao ya uchimbaji ili vijiji hivyo vipate stahiki zao kama maeneo mengine yaliyoathiriwa na shughuli za mgodi.
Katibu wa CCM Wilaya ya Geita, Cde Michael Msuya, aliwataka watumishi wa GGML wanaosimamia miradi ya CSR kuwa wazalendo na kuweka maslahi ya wananchi mbele. Alisema, “Muwe wazalendo kwenye hii nchi ili kuwasaidia wananchi wa Geita waweze kunufaika.”
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mhe. Charles Kazungu, aliwaasa madiwani na wataalamu wa halmashauri kutimiza wajibu wao katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Aliwataka pia watendaji wa GGML kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuhakikisha vijiji vyote vinavyopaswa kunufaika na mpango wa CSR vinaingizwa kwenye mipango ya mwaka 2024.
Kikao hicho kiliridhia mapendekezo ya mpango wa CSR wa mwaka 2024, ambapo GGML itachangia Shilingi Bilioni 4.3 kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi inayoendelea ili huduma zianze kutolewa kwa wananchi.
Mpango huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa mara moja ili kumaliza miradi ya viporo na kuanza kutoa huduma muhimu kwa jamii ya Geita.