📌 TPDC kusimika vituo vya CNG Mikoa ya Dar esSalaam, Morogoro na Dodoma
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuweka miundombinu ya kutumia gesi asilia (CNG) katika magari ya serikali ili yaweze kuanza kutumia nishati ya gesi.
Hayo yameelezwa leo Februari 12, 2025 bungeni jijini Dodoma na Naibu waziri wa Maliasili na Utalii Dunstan kwa niaba ya Waziri wa Nishati, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Grace Tendega aliyeuliza mkakati wa wa Serikali kuhakikisha Magari ya Serikali yanakuwa na mfumo wa nishati ya gesi.
“Mhe. Spika Ili kuwezesha Serikali kuanza kutumia magari yanayotumia gesi, Serikali imejikita kuweka miundombinu ya kuwezesha matumizi ya CNG kwenye magari ya serikali kwa urahisi”. Amesema Mhe. Kitandula.
Mhe. Kitandula ameongeza kuwa Serikali kupitia GPSA (The Government Procurement Services Agency) imeshaanza taratibu za kuweka miundombinu kwa ajili ya magari ya serikali yatakayo tumia gesi ikiwemo kufanya tathimini za athari za Kijamii na mazingira pamoja na uandaji wa michoro ya kina ya kihandisi na usimamizi wa ujenzi.
Amezielezea taratibu hizo kuwa ni kuweka miundombinu rafiki kwa magari ya serikali kuanza kutumia gesi kwenye magari (CNG).
Aidha, ili kuboresha upatikanaji wa CNG kwa mikoa iliyo katika barabara kuu kuelekea Dodoma, Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ipo kwenye hatua za manunuzi za mradi wa kuagiza na kusimika vituo vya CNG vinavyohamishika ambapo kwa kuanzia vitatu vitasimikwa Dar es Salaam, kimoja kitasimikwa Morogoro na viwili vitasimikwa Dodoma.
Hatua hizi ni sehemu ya jitihada za serikali katika kuboresha nishati rafiki kwa mazingira na kuongeza ufanisi katika matumizi ya gesi, Vituo vya CNG vitasaidia serikali na wananchi katika kufikia malengo ya matumizi ya nishati bora ikiwa Serikali inaamini kuwa matumizi ya gesi asilia katika magari ya serikali yatasaidia kupunguza matumizi ya mafuta ya petroli na hivyo kupunguza gharama za nishati.
Kwa upande mwingine, serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya gesi asilia kama njia ya kupunguza athari za kimazingira na kukuza uchumi, Hatua hii inatarajiwa kutoa suluhisho la kudumu katika sekta ya usafiri kwa kutumia nishati safi na kupunguza utegemezi wa mafuta.