Na Adery Masta
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limefanya Bonanza lake la TANO la Michezo maarufu kama VIWANGO SPORTS BONANZA kwa wafanyakazi wa shirika hilo lengo likiwa ni kuwakutanisha pamoja watumishi katika michezo ili kuboresha afya na kujenga mahusiano mazuri.
Akizungumza Leo hii Septemba 14,2024 Mgeni rasmi wa Bonanza hilo ambalo limefanyika kwenye viwanja vya Gwambina Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni , Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa amelipongeza shirika la Viwango Tanzania TBS Kwa kuendeleza tukio ili la kihistoria kwa miaka mitano mfululizo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2020 likiwa na lengo la kuboresha afya za watumishi , na kuimarisha mahusiano yao .
” Niwapongeze TBS kwa tukio ili kubwa ambalo linawaunganisha wafanyakazi wote kutoka kanda mbali mbali kwa maana michezo ni Afya , Michezo ni Fursa , na Michezo ni Ajira , na nichukue nafasi hii kuzitaka Taasisi zote za Serikali kuhakikisha zinafanya kitu kama hiki ili kuwajengea wafanyakazi wao afya iliyo bora itakayowafanya kutenda kazi kwa weledi “. amesema Bw. Msigwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TBS, Prof. Othuman Chande amewapongeza wana viwango waliojitokeza kushiriki pamoja na kushangilia katika kipindi chote cha bonanza.
“Hii itasaidia kuboresha afya zao na kujenga mahusiano mazuri kati ya watumishi, kwani utekelezaji mzuri wa majukumu yenu ya kila siku hutegemea sana afya ya mwili na akili”. Amesema
Amesema watumishi na watoa huduma wa Shirika la Viwango Tanzania wameshiriki katika michezo mbalimbali kama vile mpira wa miguu, mpira wa Pete, mpira wa wavu, kuvuta kamba na michezo ya jadi ambapo mashindano haya yameshindanishwa kiidara.
“Vilevile kupitia michezo hii watumishi hupata burudani na hupunguza msongo wa mawazo unaoweza kusababishwa na kukosa nafasi ya kufanya mazoezi au kushiriki michezo mbalimbali”. Amesema