Uongozi wa taasisi ya kusaidia watu wenye ulemavu “Foundation for Disabilities Hope (FDH) wamekabidhi tuzo ya Cheti cha pongezi kwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania TANAPA kwa kutambua jitihada za kusapoti kundi la watu wenye ulemavu na makundi maalum katika jamii ikiwemo walemavu nchini.
Hayo yamefanyika katika makao makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Arusha na kumkabidhi cheti cha pongezi Kamishna wa Uhifadhi, Shirika Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Juma Kuji kwa kutambua mchango wa shirika katika kusaidia watu wenye ulemavu na makundi maalum katika jamii ikiwemo walemavu.
Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi Bi. Mozzah Mauly pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa FDH Bw. Maiko Salali na wafanyakazi wa FDH, walitembelea ofisi hizo za TANAPA.
Aidha, kikao hicho kililenga kudumisha uhusiano uliopo kati ya TANAPA na FDH pamoja na kujadili maswala mbalimbali juu ya watu wenye ulemavu ikiwemo Kampeni “Niache Niishi; Utalii Jumuishi” ambayo itahamasisha watalii kwenda kutalii hifadhi za Taifa.
Bi Mozzah amesema dhima ya Foundation for disabilities Hope ni kuhamasisha watu wenye ulemavu kutoka ndani na nje ya nchi kutembelea vivutio vya utalii ambapo italisaidia Taifa kupata mapato ikiwa ni jitihada za kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan.
FDH wamelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kazi kubwa ya kusimamia maliasili za Taifa pamoja na kusaidia watu wenye ulemavu katika jamii.
Mkurugezi wa FDH Salali amesema “Tunajivunia sana TANAPA kwa kushika mkono makundi ya watu yenye ulemavu.”