Home Kitaifa FCT TOENI MAAMUZI KWA HAKI

FCT TOENI MAAMUZI KWA HAKI

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mkoa Dar es Salaam Dkt. Toba Nguvila ameliagiza Baraza la Ushindani (FCT) kutoa maamuzi kwa haki katika rufaa zinazowasilishwa ili kupunguza migogoro na migongano kwa wafanyabiashara na mamlaka za udhibiti

Vilevile, amelishauri Baraza hilo kutoa elimu mara kwa mara kwa wafanyabiashara ili watambue haki zao na wajue FCT ni chombo muhimu na waweze kukifikia kwa urahisi kwa kukata rufaa ambapo watakuwa hawakuridhika na maamuzi ya mamlaka za udhibiti pamoja na Tume ya Ushindani.

Dkt. Nguvila ameyasema hayo Aprili 30, jijini Dar es Salaam wakati akifungua semina iliyolenga kutoa elimu kwa wadau wa Baraza hilo kuhusu shughuli zinazotekelezwa na Baraza hilo na jinsi ya kulifikia wanapohitaji kukata rufaa dhidi ya maamuzi ya Mamlaka za Udhibiti pamoja na Tume ya Ushindani.

Naiomba FCT kusimamia haki ili iwe na tija pamoja na mambo yote hayo toa elimu mara kwa mara kwa wadau hao usikae ofisini nenda kwa wafanyabiashara kutoa elimu jinsi ya kukata rufaa kuhusu ushindani wa haki na jinsi gani watapata haki zao”. Amesema Dkt. Nguvila

Aidha, amebainisha kuwa FCT inawajibu wa kutoa suluhu ya maamuzi mbalimbali yanayolalamikiwa na walaji na kuwataka wafanyabiashara kutumia Baraza hilo ili kupata haki zao.

Kwa upande wake Msajili Mstaafu wa Baraza hilo Mhe. Renatus Rutta amesema FCT ni chombo huru cha kimahakama kilichoanzishwa na Serikali chini ya Sheria ya Ushindani Namba 8 ya mwaka 2003 .

Aidha, amebainisha kuwa FCT ina jukumu la kupokea, kusikiliza na kuamua kwa haraka rufaa zitokanazo na mashauri ya ushindani yatokanayo na maamuzi yanayofanywa na Tume ya Ushindani FCC na Mamlaka za udhibiti ambazo ni EWURA, TCAA TCRA, LATRA NA PURA.

Amesema Baraza hilo lipo kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapata haki zao wanazostahili na kamwe wasifikie. hatua ya kukwama, kwa kuwa maamuzi ya Baraza hilo ni ya mwisho.

Amesema tangu kuanzishwa kwa Baraza hilo tayari limepitia mashauri 442 na kati ya hayo mashauri 429 yametolewa maamuzi ambayo ni sawa na asilimia 97. Huku mashauri mengine yanaendelea kupokelewa na kusikilizwa na watu wamekuwa wakipewa haki zao zinazostahili.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariokoo, Bw. Martin Mbwana amesema semina iliyoandaliwa na FCT ni nzuri na imewapa mwanga katika ushindani wa biashara na jinsi ya kupata haki zao.

Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Yusuph Yenga amesema semina iliyotewa na Baraza hilo ilikuwa nzuri Na wamepata elimu na baraza hili lina umuhimu kwenye ukuaji wa biashara na uchumi.

Naye Katibu wa Umoja wa Wanawake Wafanyabiashara Machinga Complex Bi Gloria Mattoke amesema elimu waliyopata itawasaidia kuwa mabalozi wa wazuri kwa jamii kuwaelewesha kazi za Baraza hilo katika kuhakikisha ushindani wa haki unapatikana

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!