Shirika la The Foundation For Civil Society FCS limetia saini makubaliano ya ubia kati yake na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) kutekeleza mradi wa miaka mitatu wa kuwawezesha kiuchumi makundi maalum ya wanawake, Vijana watu wenye Ulemavu.
Akizungumza katika hafla fupi yakutia saini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Justice Rutenge amesema kuwa Mkataba huo unakwenda kuhakikisha fursa mbalimbali zinazopatikana katika Taifa,haziachi nyuma makundi maalum.
“Tunaingia makubaliano na SIDO ili kuwezesha makundi haya kutumia vizuri zaidi fursa mbalimbali zinazopatikana katika Shirika hili, ambalo ni muhimu sana katika maendeleo ya Viwanda, Ujasiriamali na uzalishaji mali kwa ujumla” amesema Rutenge.
Ameeleza kuwa kwa muda mrefu FCS toka kuanzishwa kwake imekuwa wakifanyakazi zilizolenga kutetea haki, katika mpango mkakati wake, wameweka haki za uchumi kama sehemu muhimu ya kazi zake ikiwemo kuhakikisha fursa zinazopatikana katika ngazi mbalimbali zinawafikia walengwa, ili kuongeza thamani katika shughuli zao.
Kwa upande wake wa FCS Charkes Kainkwa, amesema mradi huo wa miaka mitatu umefadhiliwa na TRADEMARK AFRICA, unalenga kuzalisha ajira kwa makundi maalum ili kujiongezea kipato, nakwamba kwa kushirikiana na SIDO kutawawezesha wajasiriamali kupata mafunzo yatakayopelekea kuzalisha bidhaa zenye ubora.
“Lengo la kwanza la mradi huu ni kufanya mafunzo kwa wakina mama, vijana na watu wenye ulemavu wapatao 100, lakini tunaweka mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu wa macho kupata mafunzo kwa njia rahisi kupitia vifaa vya nukta nundu”
“Kwakupitia SIDO tutawaunganisha na taasisi mbalimbali za Serikali ili bidhaa zao ziweze kutambulika na kuweza kuuza kwenye maduka makubwa na masoko mbalimbali” amesema Kainkwa.
Kwa upande wake Meneja wa SIDO Mkoa wa Dar es Salaam, Hopeness Elia, amesema muungano uliopo kati yao na FCS unaenda kuongeza nguvu na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuiwezesha jamii kufikia malengo ya kiuchumi.
Ameeleza kuwa FCS wana uzoefu mkubwa katika maeneo mbalimbali nakwamba anaamini kupitia wao wataweza kufikia malengo na kuyawezesha makundi hayo kufikia ndoto zao.
“Leo tunaanza mwanzo wa kutembea pamoja na FCS, na kunakwenda kutatua changamoto za kutokuwa na manyo za kufundishia ambayo ndio mwongozo utakaowasaidia watu wenye ulemavu, hivyo tutashirikiana na FCS ili kuwa na vitabu maalum vya kufundishia walemavu hasa wale wakuona ili viweze kutumika maeneo mbalimbali hapa nchini.
“Kwa kuungana na FCS tutatengeneza ajira kwa makundi haya kupitia mnyororo wa thamani katika uzalishaji na kuwasaidia kuongeza kipato, pia tunalenga watu chini ya umri wa miaka 35 kwa wanawake, na viajana miaka 34, kwa upande wa watu wenye ulemavu hakuna ukomo wa umri kwani tunahitaji kusaidia watu wengi zaidi kwenye kundi hili” amesema Elia.