Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB) imevitaka vyuo vyote vinavyotoa taaaluma ya uhandisi nchini kuhakikisha inaitumia kimafunzo miradi ya kimkakati inayoendelea kujengwa kwa lengo moja la kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo.
Akizungumza Dar es Salaam Leo, Msajili wa Bodi ya Usajili Mhandisi Bernard Kavishe alisema kwa kufanya hivyo mbali na faida nyingine kutawasaidia wanafunzi hao kujengewa uelewa wa haraka kuhusu miradi hiyo hatua ambayo itawafanya kuwa wahandisi bora.
“Tunaviagiza vyuo vyetu, vione umuhimu wa kwenda moja kwa moja katika miradi, tuna miradi mikubwa kama ya Bwawa la Nyerere, Ujenzi wa Reli ya ‘SGR’ na mingine mingi huko kuna utaalamu wa moja kwa moja, wajifunze ili baadae tuweze kupata wahandisi wazuri pamoja na mafundi sanifu kwa ajili ya miradi yetu” amesema Kavishe
Aidha alisema kupitia miradi hiyo, wakuu wa vyuo hivyo pia wanaweza kupata vitu na mawazo mazuri yanayowezwa kuingizwa katika mitaala ya ufundishaji na hivyo kuongeza tija katika taaluma ya uhandisi nchini.
Alisema kwa kufanya hiyo pamoja na mambo mengine kutawapa uwezo wahandisi wa hapa nchini kuchukua kazi za miradi mbalimbali inayotangazwa nchini na kuitekeleza na hivyo kuachana na dhana ya kuwategemea wahandisi na wakandarasi kutoka nje ya nchi.
Aidha katika hatua nyingine Msajili huyo alisema kwa sasa wanaangalia namna bora ya kuongeza idadi ya mafundi sanifu nchini kwa kuweka utaratibu mzuri utakaowafanya wajisajili kwa wingi tofauti na ilivyo sasa.
Alisema mbali na mpango wa kufanya mabadiliko ya kikanuni ya sheria za usajili kwa ajili ya kuwawezesha mafundi sanifu hao kujisajili kwa wingi, pia ERB ipo katika mpango wa kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya kazi zao ili kuwavutia kujisajili.
Alisema kwa sasa idadi ya mafundi sanifu waliosajiliwa nchini haizidi 2000 huku uhitajika wao katika sekta ya ujenzi ikiwa kubwa huku akitoa wito kujitokeza kwa wingi kujisajili.