Naibu Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe Mhandisi Kundo Andrea Mathew (Mb) ameyataka Mashirika ya Posta ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuchangamkia fursa za mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani kwa sasa ili sekta hiyo iweze kutoa huduma bora zinazokidhi matakwa ya wateja.
Mhandisi kundo ameyasema hayo leo tarehe 2 Novemba 2022 katika Hoteli ya Mount Meru, Arusha, wakati akifungua Jukwaa la kwanza la watoa huduma wa Sekta ya Posta na Usafirishaji, lilioandaliwa na Shirika la Posta Tanzania kwa kushirikiana na Jumuiya ya Mawasiliano kwa Nchi za Afrika Mashariki (EACO), huku likihusisha Mashirika yote ya Posta kutoka nchi za Afrika mashariki.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnaye(Mb), Mhandisi Kundo ameeleza kuwa jukwaa hilo lenye lengo la kuwakutanisha pamoja wadau wa sekta ya posta na kubadilishana uzoefu, waangalie namna bora zaidi ya kuboresha huduma za posta Kwa kuondoa changamoto ndogo ndogo zinazoikumba sekta ya Posta hasa baada ya utandawazi na teknolojia mpya na kujikita kwenye Biashara mtandao na huduma za fedha huduma jumuishi za kifedha Kwa kufanya mabadiliko mahsusi ya kidijitali.
Mhandisi Kundo aliongeza kuwa, jukwaa hilo ni la kwanza kwa Mashirika ya Posta ya Jumuiya hiyo liwe chachu ya kutoa huduma huduma za posta zilizoboreshwa na kuwafikia wananchi wengi kwa haraka, ufanisi na kwa gharama nafuu kupitia teknolojia za kisasa.
“Napenda kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri na rafiki sana ya kidiplomasia yanayotoa nafasi Kwa taasisi hizi kukutana Kwa uhuru na kujadiliana namna ya kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakabili watoa huduma mbalimbali katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, na hii inatokana na namna ambavyo Mh Rais Samia amekuwa kinara wa kuhakikisha mifumo na miundombinu ya mawasiliano nchini inazidi kurahisishwa na kuboreshwa kwa ajili ya maslahi ya wananchi” alisema Mhandisi Kundo.
Vilevile, mhe. Kundo alitumia nafasi hiyo kulipongeza Shirika la Posta Tanzania kwa mabadiliko mengi ya kidijitali ambayo Shirika hilo inayafanya kwa sasa katika huduma zake ikiwemo uwepo wa Posta kiganjani ambayo ni mpya inayounganisha hduma zote za Posta Tanzania kigajanja kwa mteja. Hivyo anajivunia sana kwa Tanzania kupata fursa ya kuandaa jukwaa hilo la kwanza kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Naye Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Mawasiliano ya Afrika Mashariki, Dkt. Alli Yahaya Simba amesema kuwa lengo la jukwaa hilo ni kuinua na kuipa mwelekeo sekta ya Posta ya Afrika Mashariki, kwani kuna fursa nyingi sana kwenye sekta ya usafirishaji, mabadiliko ya kidijitali pamoja na biashara mtandao.
Dkt. Simba amesema kuwa, kupitia Jukwaa hilo wadau wa Sekta ya Posta watapata nafasi ya kuzungumzia namna Sekta ya Posta itakavyosaidia wananchi wake kiuchumi hasa kwa kuzingatia kuwa huduma za kifedha na biashara mtandao ni moja ya majukumu ya Masharika ya Posta.
Aliongeza kuwa, EACO iko katika mchakato wa kuifanya iwe Taasisi Kitovu cha TEHAMA kwa Nchi za Afrika Mashariki ili kuhakikisha yale matunda yanayotokana na Sekta ya Posta yanaonekana na kuwafikia wananchi wa Jumuiya hiyo kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Ndugu Macrice Mbodo amesema kuwa, ni heshima kubwa kwa Shirika la Posta Tanzania kwa kushirikiana na EACO kuandaa Jukwaa hilo la kwanza kwa Posta za Afrika Mashariki ambalo halikuwahi kufanyika hapo kabla.
“Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kupitia mamlaka zake kwa kuturuhusu sisi kuandaa na kufanya mkutano huu. Mageuzi ya posta yetu ya Tanzania yanayoendelea kufanyika kwa sasa yamekuwa kivutio kwa Posta zingine za Afrika Mashariki na kupitia mkutano huu tutatumia fursa hii kuonyesha namna ambavyo tunatoa huduma zetu kidigitali ili na wenzetu waweze kupata uzoefu kupitia kwetu” Amesema Postamasta Mkuu Mbodo.
Aidha ameeleza kuwa, wameona umuhimu wa kukaa pamoja kama Wakuu wa Posta wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kutafakari namna ambavyo Taasisi hizo zitaweza kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na kushiriki katika mchango wa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.