Na Magreth Mbinga
Vijana wamepewa wito wa kufanya mazoezi kwaajili ya kujenga afya ya mwili na akili ili kujenga taifa la watu wenye maendeleo na kukuza uchumi kwa ujumla .
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa huduma ya vijana Mashariki na kati Mchungaji Lupakisyo Mwakasweswe katika mbio za Una Mungu Fun Run iliyoandaliwa na kikundi cha Ellen Evangelistic Singers zilizoambatana na ugawaji wa vitabu vya neno la kutoa moyo.
“Mazoezi ni kitu muhimu sana katika maisha ya mwanadamu sababu Mungu ameumba mwili huu ili ukue unapofanya mazoezi viungo viongezeka na inatia hamu ya kula kwa watu ambao walikuwa hawana hamu ya kula” amesema Mchungaji Mwakasweswe.
Pia Mkurugenzi wa Ellen Evangelistic Singers Prof Pendo Malangwa amesema ilikuwa siku maalumu sana kwani ni moja ya maadhimisho ya miaka kumi ya Ellen Singers waliandaa mbio ambazo wameziita Una Mungu Fun Run sababu ndani take kulikuwa na tukio la kutoa msaada wa vitabu ambavyo viligaiwa bure kwa watu .
“Tuliitisha marafiki mbalimbali ambao walijiandikisha kukimbia na wengine walitoa sadaka kwaajili ya kununua vitabu ili tuweze kuvigawa katika Jiji la Dar es Salaam na leo ndio ilikuwa kilele cha shughuli yote kwa ujumla watu walikimbia na tuligawa vitabu” amesema Prof Malangwa.
Aidha Prof Malangwa amesema vitabu ambavyo walichagua kugawa ni kitabu cha jipatie amani moyoni na pendo lisilo kifani kwakuwa wanatambua misukosuko ya Dunia ambavyo watu wanapitia wanahitaji faraja na kutiwa moyo Ellen Singers kama kikundi cha uimbaji wamekuwa wakifanya kazi ya kutia moyo wajane,yatima ,walemavu na watu wenye changamoto mbalimbali.
Sanjari na hayo Mshindi wa kwanza wa Una Mungu Fun Run amepatiwa pesa taslimu shilingi laki tano,kombe cha ushindi , kikombe cha chai na cheti cha ushiriki , mshindi wa pili amepatiwa pesa taslimu shilimgi laki tatu,kikombe cha chai pamoja na cheti cha ushiriki na mshindi wa tatu amepata pesa taslimu shilingi laki mbili,kikombe cha chai na cheti cha ushiriki.
Sanjari na hayo moja kati ya washiriki wa mbio hizo Prince Emmanuel amesema zoezi hilo limewaleta na kuwakutanisha na watu tofauti wakakimbia pamoja mara nyingi huwa wanakutana katika mitandao ya kijamii lakini Ellen Singers wameweza kuwaunganisha .
“Watu wengi tunachangamoto ya kuto kusoma vitabu lakini ili uweze kupata maalifa zaidi lazima usome kitabu Ellen Singers kwa kuliona hili ndio maana wametoa vitabu ili vizidishe maarifa kwa wote ambao watavisoma” amesema Prince.